Pinda: Mishahara ya wabunge haitoshi
Thursday, 30 April, 2009, 13:18
Tanzania Daima 30.04.2009 (http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=4575)

WAKATI Bunge zima likimwandama Mbunge wa Karatu, Dk. Wilibrod Slaa (CHADEMA), kutokana na msimamo wake kuwa posho za wabunge ni kubwa na kutaka zipunguzwe, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameungana na wabunge wengine kwa kusema kuwa posho hizo ni ndogo na kutaka ziongezwe.

Ingawa hakutaja jina, lakini kauli hiyo ya Waziri Mkuu imeonekana dhahiri kumjibu Dk. Slaa anayetaka mishahara na posho za wabunge zipunguzwe, kwamba ni kubwa mno ukilinganisha na watumishi wengine wa umma.

Pinda aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua mpango mkakati wa Bunge wa miaka mitano, wenye nia ya kulifikisha Bunge katika kiwango cha juu cha ufanisi.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, Pinda alitumia mwanya huo kuchomeka suala la posho za wabunge, ambalo limekuwa agenda kubwa katika mkutano wa 15 wa Bunge unaomalizika leo.

Akielezea hatua ambazo serikali imekuwa ikizifanya kwa upande wa Bunge, Pinda ambaye aliorodhesha hatua kadhaa za kuboresha maslahi ya Bunge, alisema lengo la serikali ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa sasa bado ni ndogo.

“Lengo la serikali kwa Bunge ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa kweli kwa sasa hazifikii stahiki, lengo ni kuhakikisha Bunge linaboreshewa maslahi ili liweze kufanya kazi yake stahiki na kwa kiwango cha kuridhisha,” alisema Pinda.

Awali, akizungumzia malengo makubwa saba ya mpango mkakati huo, alisema moja ya malengo hayo ni kuboresha maslahi na stahiki za wabunge ili kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo.

Mbali na malengo hayo, mengine ya mkakati huo ni kuboresha muundo na utendaji wa ofisi za Bunge ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji, pia kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya sekretarieti ya Bunge.

Limo pia suala la kukuza na kuimarisha ushiriki wa Bunge kuwafikia wadau mbalimbali kupitia mikutano, machapisho, vyombo vya habari na njia nyingine ya mawasiliano, pamoja na kukuza na kuinua vipaji vya wabunge.

Kwa upande wa serikali, mbali na malengo ya kuboresha maslahi na posho za wabunge kwa kuzingatia mazingira ya utendaji wao wa kazi, na hali ya uchumi, Pinda pia aliyataja malengo mengine kuwa ni kuwezesha Bunge kuwa na ukumbi mzuri wa kisasa unaotosheleza mahitaji, lengo ambalo kwa sasa tayari limekwishatekelezwa.

Kwa mujibu wa Pinda, lengo lingine ni kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa Bunge ambao ulianza kutumika mwaka 2007/08, kuwashirikisha katika ziara za nje za viongozi wa kitaifa, lakini pia kuharakisha ujenzi wa ofisi za wabunge katika majimbo yao.

Tangu alipotoa kauli hiyo akiwa kwenye moja ya mikutano ya chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa akiandamwa na wabunge wenzake katika mkutano huu wa 15, wakipinga hoja hiyo kwa madai kuwa inawachonganisha wabunge na jamii.

Hali hiyo ilisababisha Dk. Slaa afikie hatua ya kuzomewa mara kadhaa kila jina lake linapotajwa kwenye vikao vya ndani na nje.

Mbunge huyo, hata hivyo, alisisitiza kwamba anasimama katika hoja zake, ikiwamo ya posho za wabunge kutaka kutazamwa upya.

Alisema ataendelea kuisimamia hoja hiyo kwa sababu anataka kuwapo kwa uwazi katika mishahara wanayolipwa viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge.


[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
TLP:Mutungirehi, Kinanda wapewa vyeo
Tuesday, 28 April, 2009, 07:24
Kutoka Magazetini

HALI imezidi kuwa tete ndani ya TLP, ambapo sasa kundi la wajumbe 750 wa mkutano mkuu wametangaza kutomtambua Mwenyekiti wa chama hicho Augustine Mrema, huku wakimtangaza Joram Kinanda kuwa Makamu Mwenyekiti na Benedicto Mutungirehi kuwa Katibu Mkuu wa TLP.

Hali hiyo imeibuka siku moja tu tangu chama hicho kilipofanya uchaguzi wake, uliomuweka Mrema madarakani. Hata hivyo, mizengwe, fitna na ubabe vinadaiwa kugubika uchaguzi huo, huku Mrema akituhumiwa kutumia ubabe kuwaengua wapinzani wake.

Mbali na wajumbe hao kutangaza kutomtambua Mrema, pia wamedai kuwa ni ‘fisadi papa’ wa kisiasa hivyo, hastahili kukiongoza chama hicho.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, jana, mwenyekiti wa kamati ya muda ya TLP, Macmillan Lyimo, alisema maamuzi hayo yamefikiwa na wajumbe, baada ya kufanya mkutano mkuu wa chama hicho katika ukumbi wa Millennium.

Alisema wajumbe hao zaidi ya 750 walinyimwa haki ya kikatiba kushiriki uchaguzi mkuu huo, ambao ulimuweka madarakani Mrema kinyume na utaratibu.

“Wajumbe waliomchagua Mrema na kumuweka madarakani ni wa halmashauri kuu, na si wajumbe wa mkutano mkuu…haiwezekani Mwenyekiti achaguliwe na wajumbe 120, ni kinyume na katiba ya chama, na lazima tumpeleka Mrema mahakamani,” alisema Lyimo.

Alisema, Katiba inatamka wajumbe 1,407 ndiyo wanaopaswa kushiriki uchaguzi, lakini alibadili katiba na kutangaza wajumbe waliotakiwa kuwa ni 163, na walioshiriki uchaguzi huo ni 123.

Kutokana na hatua hiyo, wajumbe hao chini ya Lyimo, walifanya uchaguzi wa kutafuta viongozi watakaoiongoza TLP, ambapo Kinanda aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na Mutungirehi kuwa Katibu Mkuu.

Katika uchaguzi uliofanyika juzi na kumuingiza madarakani kwa mara nyingine tena Mrema, wajumbe kutoka mikoa ya Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara, Kagera, Pwani hawakuhudhuria kikao hicho.

Gazeti hili lilipowasiliana na Mrema juu ya hali hiyo, alisema yeye ni mwenyekiti halali wa TLP, na kwamba hawatambui Mutungirehi na Kinanda.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Rais Kikwete atengua uteuzi wa DC wa Kishapu
Sunday, 26 April, 2009, 07:59
Na Mwananchi (25.04.2009)

RAIS Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wa Mkuu mpya wa Wilaya ya Kishapu, Anatory Choya muda mfupi baada ya kumtangaza na badala yake akamteua mwingine, Abdul Suleiman Lutavi.

Habari zilizopatikana zinaeleza kutenguliwa kwa uteuzi wa Choya ambaye ni mbunge wa zamani wa Biharamulo Magharibi mkoani Kagera, kutokana na kukamatwa na Takukuru na kufunguliwa kesi ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Biharamulo mwaka jana, nafasi ambayo alishinda.

Kesi yake namba 270 ya mwaka 2008 inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo na wiki iliyopita, Aprili 17 mwaka huu ilitajwa na inatarajiwa kutajwa tena Mei 11 mwaka huu.

Jumatatu wiki hii wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Shinyanga, pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwake walipigwa na butwaa baada ya kushuhudia akiapishwa Lutavi badala ya Choya.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dk Yohana Balele alimwapisha Lutavi na kuwafanya watu kuhoji kimya kimya nini kilichofanya Choya kushindwa kuapishwa na hakuna maelezo yaliyotolewa.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zinaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, alitengua uteuzi wa Choya kutokana na taarifa zilizoifikia ikulu kuwa Choya, anakabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani.

Hizi ni dalili nzuri. Je, wewe una maoni yapi ?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Mfanyabiashara maarufu Reginald Mengi ajitoa mhanga kwa mafisadi
Saturday, 25 April, 2009, 10:17
Na Mwananchi 23.04.2009

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Reginald Mengi jana aliamua kujitoa muhanga alipotangaza majina ya wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia ambao anadai kuwa ni mafisadi papa wanaoiba mabilioni ya fedha za wananchi na kutaka wachukuliwe hatua kwa madai kuwa wataiyumbisha na kuitingisha nchi.

Kati ya wafanyabiashara waliotajwa na Mengi, wawili wamefunguliwa mashtaka ya tuhuma za wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), wengine wakiwa wameshatajwa kwenye kashfa mbalimbali, zikiwemo za zabuni ya utoaji umeme wa dharura ya Richmond Development na uuzwaji wa jengo la Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mengi, ambaye anamiliki kampuni ya IPP yenye kampuni mbalimbali zikiwemo za habari na vinywaji, alitaja wafanyabiashara hao watano akisema kuwa ndio papa kwa ufisadi lakini akasema idadi ya mafisadi wanaofilisi nchi hawazidi 10.

"Wanaotuhumiwa kuwa mafisadi papa wanahusishwa na karibu kila kashfa kubwa hapa nchini zikiwepo kashfa za Richmond, EPA, Dowans, helikopta na magari ya jeshi, ndege ya rais, rada, NSSF, Bahati Nasibu ya Taifa, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na kadhalika," alidai Mengi katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya kwenye ofisi yake jijini Dar es salaam.

Kati ya wafanyabiashara hao watano ambao Mengi alidai ni mapapa wa ufisadi, wamo Rostam Aziz, Yusuf Manji na Jayantkumar Chandubhai Patel (Jeetu Patel), ambao Mwananchi ilipata nafasi ya kuzungumza nao kuhusu tuhuma hizo za Mengi.

Hata hivyo, Mengi hakuwa tayari kutoa vielelezo kuthibitisha madai yake, lakini akasema iwapo watamshtaki mahakamani na wafanye hivyo kwa kuwa huko ndiko haki inakopatikana.

Mengi alirusha tuhuma nyingi kwa watu hao ambao alidai kuwa wamecharuka baada ya Rais Jakaya Kikwete kuamua kupambana nao na hivyo wameamua kupambana na yeyote anayemsaidia mkuu huyo wa nchi katika vita hiyo.

"Jitihada kubwa za Mhe. Rais za kuleta maendeleo na maisha bora kwa kila Mtanzania zinazoofishwa na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa. Bado Watanzania wengi wanaandamwa na umaskini mkubwa; hawajui hata mlo mmoja kwa siku utatoka wapi," alidai Mengi ambaye pia alitoa taarifa ya maandishi aliyoisaini.

"Cha kusikitisha ni kuwa pale Mtanzania mwema mwenye uwezo anaposaidia jamii kuondokana na umasikini, mafisadi wanapiga kelele kuwa misaada ya aina hiyo ina agenda. Wanapinga kwa kuwa wanataka Watanzania wafe na njaa na matatizo mengine."

Mengi alikwenda mbali zaidi na kudai mafisadi anaowatuhumu wanaweza wakaunga mkono matatizo yanayotokana na Deci, taasisi inayoendesha mchezo wa kuchangisha fedha na kulipa maradufu na Watanzania kubakia "wakifukuzana na wachungaji bila ya kujiuliza ni kina nani hasa wanachochea vurugu".

Wakiongea na Mwananchi, watu hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi hawakutaka kujibu kwa kirefu na badala yake walimtuhumu mwenyekiti huyo mtendaji wa IPP kuwa ana wivu, fitina chuki na ambaye ameshindwa kuendesha nyumba na biashara zake, huku mwingine akieleza kuwa anatumia haki yake ya kidemokrasia ya kutoa maoni yake.

"Mengi... (si mstaarabu)," alisema Manji ambaye anamiliki kampuni ya Quality Group. " Biashara zake zimemshinda ndio maana anazungumza ovyo."

Rostam Aziz, ambaye ni mbunge wa Igunga anayejishughulisha na biashara mbalimbali za miradi mikubwa ya ujenzi, uchimbaji na habari, alimuelezea Mengi kama mtu ambaye analingana kwa umri na baba yake mzazi na hivyo hawezi kubishana naye.

Lakini akasema: "Mengi amejaa chuki, wivu na fitina. Sina cha kumsaidia isipokuwa kumuombea Mungu ili amsaidie kwa kumpuuzia hayo maana ni adhabu kwa nafsi yake mwenyewe. Kwa malezi niliyopata, siwezi kubishana na mzee."

Jeetu Patel naye alisema haoni busara kujibizana na Mengi na kwamba alichofanya mwenyekiti huyo wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda (CTI) ni kutumia haki yake ya kidemokrasia ya uhuru wa kuongea.

“Hayo ni matatizo yake," alisema Patel, ambaye anakabiliwa na kesi ya tuhuma za wizi wa fedha za EPA. "Amewaita waandishi kuzungumza nao... sikumsikia lakini ninachoweza kusema ni kwamba anatumia uhuru wake wa kujieleza.

"Binafsi sijui chochote kuhusu hizo tuhuma za Mengi dhidi yangu, ila anayo haki ya kusema chochote. Nina mambo mengi ya kufanya hivyo sioni kama itanisaidia kwenye biashara zangu za kila siku kuanza majibizano na Mengi."

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mengi alidai kuwa watu hao aliowataja si tu kwamba wanaiba rasilimali za Tanzania, bali pia wanaiba muda wa Watanzania.

"Badala ya kutumia muda katika shughuli za maendeleo, tunajikuta tukitumia muda mwingi kupambana nao na hawatingishiki," alidai Mengi. "Badala yake wanatumia fedha walizotuibia kuanzisha magazeti ya kujenga kiburi cha kutudharau, kututukana na kutunyanyasa. Inakuwa kesi ya mwizi kumkimbiza na kumpiga aliyeibiwa.

"Hata sasa hivi, mafisadi papa wanaendelea kutumia uwezo wao wa kiuchumi uliotokana na wizi wa rasilimali za nchi yetu kushawishi na kupata miradi mikubwa mikubwa kwa kutumia majina tofauti tofauti huku wakipuuza kabisa kelele za wananchi kuhusu ufisadi wao.

Alisema ni muhimu wananchi wakajiuliza hawa mafisadi wanapata wapi ujasiri wa majigambo, dharau na nguvu za kutukana na kunyanyasa watu.

Alisema mafisadi papa ni lazima wajue kwamba iwapo wapambanaji wa ufisadi watapata madhara kwa njia yoyote hapa nchini au nje ya nchi, wananchi wa Tanzania watawawajibisha.

"Ni lazima Watanzania wote tuone kwamba sasa tumefika mahali pa kusema imetosha," alidai Mengi.


[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Dk. Slaa azomewa bungeni
Saturday, 25 April, 2009, 09:58
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, jana alilazimika kuwasihi na kuwaomba wabunge kuwa watulivu, baada ya ukumbi kulipuka wakimzomea Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA).

Kizaazaa hicho kilianza baada ya Spika Sitta kutangaza kuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Dk. Slaa alikuwa ameomba kukutana na wajumbe wa kamati hiyo jana saa tano asubuhi.

Kutajwa kwa jina la Dk. Slaa kulizusha kelele za kumzomea mbunge huyo, jambo lililomfanya Spika kushindwa kuendelea na matangazo ya shughuli za asubuhi.

“Waheshimiwa wabunge naomba utulivu, najua misimamo ya Dk. Slaa imesimama katika upotoshaji, lakini yeye (Dk. Slaa) ni mwenyekiti wa kamati na ana haki ya kuitisha vikao,” alisema Spika Sitta.

Dk. Slaa amekuwa akishutumiwa na wabunge wenzake kutokana na msimamo wake kwamba, wabunge wanalipwa mshahara mkubwa ikilinganishwa na mishahara ya wafanyakazi wengine wa kawaida.

Msimamo huo wa Dk. Slaa umepingwa na wabunge wengi, wakiwemo wa upinzani wakidai kitendo chake cha kusimama kwenye majukwaa ya siasa na kutangaza mshahara wa wabunge ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Baadhi ya wabunge walipendekeza Dk. Slaa kutokana na kitendo chake cha kuwachonganisha wabunge na wananchi, aondolewe katika nafasi ya mwenyekiti wa kamati hiyo.

Juzi iliripotiwa kwamba, Dk. Slaa alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge, wakiwemo kutoka kambi ya upinzani kumshambulia kutokana na kutangaza mshahara na marupurupu ya ubunge kwa wapiga kura wake.

Imeelezwa kuwa hilo lilijitokeza katika kikao cha ndani cha wabunge, kilichofanyika baada ya kipindi cha maswali na majibu, ambapo walisema kitendo cha Dk. Slaa ni ukiukwaji wa maadili ya Bunge.

Miongoni mwa wabunge waliomvaa Dk. Slaa ni Lucas Selelii (Nzega-CCM), aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Bunge kutokana na kitendo hicho cha ukiukwaji wa maadili.

Mwingine ni John Cheyo (Bariadi Mashariki -UDP), aliyemweleza Dk. Slaa kwamba urais haupatikani kwa njia anazotumia.

Naye Anna Komu (Viti Maalumu-CHADEMA) alisema anashangazwa na ukimya wa Bunge baada ya Dk. Slaa kutoa kauli hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati wabunge wakimshambulia, Dk. Slaa alikuwa kimya.

Je, ni halali kumzomea? Pili je mishahara minono kwa wabunge tu ndiyo uwakilishi? Jadili

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Wagombea mwakani kubanwa kitaaluma
Tuesday, 21 April, 2009, 09:55
Baraza la Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) limepitisha uamuzi wa kuishirikisha Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kuhakiki vyeti vya wote wanaoomba kuwania nafasi za kisiasa ili sifa zao kielimu zitambulike.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Mayunga Nkunya, aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam, TCU imewasiliana na NEC kwa barua, ili utaratibu huo uanze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.

Nkunya alitoa taarifa hiyo wakati akizungumzia maonyesho ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na TCU yatakayoanza kesho hadi Aprili 24, mwaka huu. “Baraza letu limepitisha uamuzi ili watu wanaotaka kugombea nafasi za kisiasa, vyeti vyao vihakikiwe, ili akipita sifa ijulikane rasmi kama ni daktari basi awe daktari na si daktari feki,” alisema Profesa Nkunya.

Hatua hiyo ya tume inatokana na kilichoelezwa na Nkunya kuwa ni kukithiri kwa vyuo na vyeti bandia nchini, jambo ambalo alisema wamejipanga kulivalia njuga kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha Tanzania haiangamii kitaalamu na kitaaluma.

Alisema orodha ya vyuo visivyotambulika vya nje ambavyo Watanzania wengi wakiwamo mawaziri na wabunge wamesoma, ni ya kweli na kwamba kama kuna mtu anahisi kuonewa ruhusa kwenda mahakamani.

“Sisi TCU tumepewa jukumu na taifa hili, kuhakikisha elimu inayotolewa kwa Mtanzania inatambulika duniani kote na inatolewa na vyuo vinavyotambulika, tulitoa orodha ya vyuo feki sasa kama kuna mtu anapinga aende mahakamani,” alisema Profesa Nkunya wakati akijibu swali juu ya ukweli wa orodha ya vyuo feki iliyotolewa na tume hiyo hivi karibuni.

Akizungumzia tatizo la kughushi vyeti, alisema linazidi kukua, hali ambayo inatishia sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na uwezekano wa Tanzania kuzalisha wataalamu feki. “Tatizo la kughushi vyeti linazidi kuwa kubwa nchini hali ambayo ni hatari na haipaswi kufumbiwa macho, si siri tatizo hili lisipodhibitiwa nchi itaenda pabaya, tushirikiane tulidhibiti,” alisema.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji huyo wa TCU, katika udahili wa mwaka 2008/09 pekee, tume hiyo ilipelekewa majina ya wanafunzi zaidi ya 200 ambao vyeti vyao vinasadikiwa kughushiwa. “Hii ni hatari, tusaidiane kukabiliana na tatizo hili, tukiacha liendelee nchi yetu itakwenda pabaya na hatari yake ni kuzalisha wataalamu feki,” alisema Nkunya.

Alisema kwa sasa watu wanaoongoza kwa kupeleka vyeti vya kughushi vyuoni ni waliosoma miaka ya nyuma, hali inayoonyesha ni upungufu wa nidhamu ambao inabidi uchukuliwe hatua. Alitoa mfano wa Liberia ambayo iliacha tatizo hilo la kughushi na kuwa na vyuo feki likakua na kusema nchi hiyo imefanya elimu yake kutokuwa ya kuaminika.

“Kwa sasa hali ya Liberia kielimu ni mbaya, waziri anaweza kuanzisha chuo chake na kujipa shahada, hiyo elimu gani?” Alihoji. Profesa Nkunya aliitaka jamii isiliache tatizo hilo mikononi mwa TCU na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) pekee, bali liwe mikononi mwa kila mtu vikiwamo vyombo vya Dola, katika kupambana nalo.

“Sheria ziangaliwe, kwani kukithiri kwake kunatokana na wanaokamatwa kutochukuliwa hatua thabiti za kukomesha tabia hiyo,” alisema. Alisema katika kuhakikisha kuwa hadi kwenye ofisi watu wenye vyeti bandia wanadhibitiwa, TCU pia imejipanga kurekebisha sheria yake, ili iwe na uwezo wa kutembelea ofisi moja baada ya nyingine, kuhakiki vyeti vya watu.

Alisema imeshaanza mchakato wa kurekebisha sheria hiyo. Hivi karibuni, NECTA ilitoa taarifa na orodha ya maelfu ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya ualimu wanaotarajia kufanya mtihani wao wa mwisho mwezi huo, ambao walibainika kutumia vyeti bandia na kuwataka wawasilishe vithibitisho, vinginevyo hawataruhusiwa kufanya mtihani.

Hata hivyo, kutokana na kukithiri kwa vyeti bandia, serikali imedhamiria kupambana na watumishi waliowasilisha vyeti bandia baada ya idara zote za serikali kutakiwa kuhakikisha zinawasilisha vyeti vya watumishi wake kwa ajili ya uhakiki, mchakato ambao unaendelea hadi sasa, huku baadhi wakiachishwa kazi kutokana na kukutwa na vyeti bandia.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Dk. Wilbroad Slaa kuburuzwa kortini
Saturday, 18 April, 2009, 10:00
Na Gazeti la Uhuru

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, anatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kushindwa kulinda katiba ya chama hicho.

Hayo yalisemwa jana mjini Dar es Salaam na aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Kinondoni, Martin Mg'ong'o, aliyefukuzwa hivi karibuni.

Mng'ong'o alisema kuwa, wanasheria wanaandaa mashitaka dhidi ya Dk. Slaa na baadhi ya viongozi walioshiriki kutoa maamuzi ya kumfukuza pamoja na wanachama wengine 15 wa wilaya hiyo.

Alisema, maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika mwezi uliopita yalikiuka baadhi ya vifungu vya katiba ya mwaka 2004, kwa kutoa adhabu bila kusikiliza utetezi wa wanachama hao.

Kiongozi huyo, ambaye alisisitiza kutotambua kutimuliwa kwao, alisema kifungu cha 5.4.3 na 5.4.4 cha katiba ya chama hicho, kinasisitiza umuhimu kwa watuhumiwa kupewa mashitaka kwa njia ya maandishi na kuyajibu kwa njia hiyo kabla ya kusikilizwa na vikao vinavyohusika.

"Haya yote yamekiukwa kwa shinikizo la viongozi wa juu, yaani (Freeman) Mbowe na (Dk. Wilbroad) Slaa ambao walilalamikiwa na wanachama wale waliotaka uwazi zaidi ndani ya chama," alisema Mng'ong'o.

Alisema, kwa mujibu wa katiba na taratibu za chama chao, Dk.Slaa kama Katibu Mkuu, amepewa jukumu la kusimamia katiba na kuhakikisha haikiukwi kwa namna yoyote na si vinginevyo.

"Sasa kwa kushiriki kwake kuivunja na kuivuruga katiba na sheria, tunakusudia kumpandisha kizimbani ili ajibu tuhuma hizo...inashangaza yeye anajiita mpenda haki na kumbe ndiye mkiukaji mkubwa wa haki za wananchi," alisisitiza.

Mng'ong'o alisema kwamba, tayari ameuandikia uongozi wa chama hicho kupinga kutimuliwa kwao, na kuutaka utoe tamko la kuwarejesha kwa vile hawakukiuka katiba ya chama hicho.

Alisema, yapo madai kuwa katika kikao kilichofikia uamuzi wa kuwatimua, baadhi ya viongozi walitumia ubabe kushinikiza kuwa lazima wanachama hao watimuliwe vinginevyo wao (viongozi hao) wangeondoka CHADEMA.

"Hivyo ndivyo ilivyokuwa, mtu anadiriki kusimama na kupinga ushauri wa waasisi wa chama tena kibabe baada ya washauri hao kutaka wote tuliotuhumiwa tusikilizwe na vikao husika kabla ya uamuzi wowote," alisema

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
CCM wamejipanga-Mrema
Wednesday, 15 April, 2009, 18:45
Na habari leo

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema amekiri, kwamba Chama Cha Mapinduzi ( CCM) kina utaratibu mzuri wa kuandaa wagombea wake katika nyadhifa za juu ukiwamo urais. Mrema alisema hayo jana kwenye mahojiano katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) .

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, suala la mtafaruku ndani ya TLP, si la yeye kung’ang’ania madaraka, bali inapokuwa chama hakijaandaa mgombea madhubuti atakayeweza kuwa mtetezi mkubwa wa chama hicho, ndipo suala hilo linapojitokeza.

“Watu wanaandaliwa, kama watu wa CCM, unawasikia kuwa mwaka 2010 ni Kikwete tu, wana utaratibu … wanaandaa, hawaendi kiholela ili mradi tu umechukua fomu sijui nani …na wanajua kazi aliyofanya Kikwete na wameridhika,” alisema Mrema na kuongeza: “Wao wanafikiri kwamba si kazi ya kubughudhi tena kwa sasa … wanatamka hivyo na kwa jambo hilo huwezi kusema hiyo si demokrasia ama huo ni udikteka,” alisema Mrema.

Alishangazwa kuona wakati CCM ikijipanga vizuri namna ya kuachiana madaraka, vyama vya Upinzani hususan chama chake, jambo hilo ni tofauti kiasi cha kufikia kuwapo mtafaruku mkubwa wa kuwania madaraka. Hata hivyo alisema, hang’ang’anii madaraka ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho, bali hakuna mwanachama madhubuti kwa sasa aliyeandaliwa kukiongoza vyema chama hicho. “Akiandaliwa mtu sawa … nimewaambia Halmashauri Kuu ya Chama, kwamba sing’ang’anii uenyekiti … watu wanaandaliwa kushika nyadhifa hizi,” alisema Mrema na kuongeza:

“Mnataka Mrema aondoke … haondoki mtu mpaka chama hiki kijengwe na nijue nitamwachia nani, siwezi kukiacha chama changu barabarani, haiwezekani.” Akizungumzia nia yake ya kugombea ubunge mwakani Moshi Vijijini kwa tiketi ya TLP, alisema atafanya hivyo kutokana na kuombwa na wananchi wa jimbo hilo. Hivi sasa Moshi Vijijini inawakilishwa na Dk. Cyril Chami wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.



[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Utaratibu mpya kura za maoni CCM…
Wednesday, 15 April, 2009, 18:31
(Na Gazeti la Uhuru)

UTARATIBU mpya wa upigaji kura za maoni katika kuchagua mgombea wa udiwani na ubunge, utasaidia kuwaondoa 'madalali' wa wagombea ambao ndio chanzo cha rushwa na kuanzisha makundi ndani ya wanachama wa CCM, imeelezwa.

Hayo yalisemwa juzi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Dk. Makongoro Mahanga, wakati akizungumza na Jumuia ya Wazazi katika kata ya Vingunguti, Dar es Salaam.

Alisema uamuzi uliopitishwa wa wanachama kuwapigia kura za maoni wagombea wa nafazi hizo, utasaidia katika kumaliza makundi ambayo mara nyingi husababishwa na 'madalali' wa wagombea ambao kazi yao kubwa huwa ni kuchonganisha wanachama kwa lengo la kufanikisha mgombea wanayemtaka kuchaguliwa.

"Madalali' kazi yenu imekwisha utaratibu huu hauwafai kabisa ni vyema sasa mkatafuta kazi nyingine, haitawezekana mkawashawishi wanachama wote kuanzia ngazi ya tawi, eti wamchague fulani kigezo kikubwa kitakachotumika hapa ni kitu gani unawafanyia wananchi," alisema Dk. Mahanga.

Alisema utaratibu huo utasaidia kumaliza tatizo la rushwa ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu, na kwa kiasi kikubwa lilikuwa likisababishwa na ‘madalali’ hao.

Dk. Mahanga alisema kuwa, kufanyika kwa utaratibu huo kutasaidia kupanua demkorasia, na kuondokana na kura kupigwa na kikundi cha watu wachache.

Alionya tabia ya baadhi ya wanachama wanaowahujumu viongozi walioko madarakani, katika kazi zao mbalimbali na kusema watakaobainika kufanya hivyo, Chama kitawachukulia hatua kali.

"Kuna wanachama wanajiona wana kazi ya kuhujumu viongozi walioko madarakani ili wasitimize majukumu yao, hili tumeligundua na watakaoendelea hatua kali zitachukuliwa.

Acheni kila kiongozi afanye kazi zake kwa uhuru, mimi kama mbunge nina uhuru wa kutembelea jimbo langu, bila kizuizi chochote hivyo hakuna mtu wa kunizuia, kinachotakiwa ni kuwatumikia wananchi waliotuchagua na si kazi ya kuhujumiana," alisema Dk. Mahanga.

Akizungumzia makundi ndani ya Chama, aliwataka kujenga utamaduni wa kuwasema hadharani wanaoendeleza makundi kupitia vikao halali vya CCM.

"Nina mfano mzuri katika kata zangu, kata ya Tabata ndio inayoongoza kwa makundi, lakini hili tutapambana nalo mpaka limalizike, hatutakubali kubaki na watu wanaokiharibu Chama kwa maslahi yao binafsi," alisema Dk. Mahanga.


Je, wewe una maoni yapi?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Bunge lakataa taarifa ya Ngeleja
Wednesday, 15 April, 2009, 12:07
(Habari Leo 15.04.2009)

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imemwagiza Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuipelekea taarifa inayojitosheleza kuhusu mgodi wa Williamson Diamond Limited (WDL), ikiwa ni pamoja na kueleza bayana hatma ya mchakato wa kufahamu uhalali wa deni la dola milioni 87.5 za Marekani.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya kamati hiyo zilibainisha jana, kuwa hatua ya kumtaka Waziri kupeleka tena taarifa baada ya aliyowasilisha jana katika kamati hiyo kutojitosheleza licha ya kupokewa, zilitokana na mambo mbalimbali ikiwamo kutobainisha wazi suala la Kampuni mpya ya Petra Diamonds Limited kumiliki kile alichodai ni asilimia 75 ya hisa.

“Sasa kama Waziri analeta taarifa kwa kamati na inaeleza masuala ya ‘indirectly’ katika kumiliki hisa asilimia 75, hii inahitaji ufafanuzi zaidi ili tupate kitu cha kutoa bungeni, hivyo tumemtaka alete taarifa yenye ufafanuzi wa masuala hayo pamoja na kampuni itakayochunguza uhalali wa deni la dola milioni 87.5,” alieleza mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Kampuni ya Petra yenye makao yake Afrika Kusini ilikubaliwa na serikali kumiliki (si moja kwa moja) hisa asilimia 75 baada ya kuinunua Kampuni ya Willcroft (Kampuni tanzu ya De Beers) kwa dola milioni 10 kwa masharti ya kutambua mikataba iliyopo na deni hilo linalozidi Sh bilioni 100. Katika ubia huo, serikali inamiliki asilimia 25 ya hisa.

Habari zaidi zilieleza kuwa pamoja na taarifa ya Waziri kuonyesha kuwa Petra imechunguzwa na kukubalika na Baraza la Mawaziri kuwa inafaa kuendelea kumiliki sehemu hiyo ya hisa, mjadala mkali uliibuka jana ukimtaka Waziri aeleze kwa kina, faida ambayo serikali na Watanzania wataipata kutokana na mbia mpya.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ngeleja kwa kamati hiyo ambayo nakala iligawiwa kwa waandishi na kisha kutolewa nje ili kikao kiwe cha faragha, faida itakazopata serikali kupitia mradi wa upanuzi wa uzalishaji ili kurekebisha mwenendo mbaya wa fedha uliosababisha deni hilo, ni ajira kwa wananchi na misaada ya kijamii katika maeneo yanayozunguka mgodi.

Akifafanua kuhusu mjadala wa suala hilo kwa waandishi wa habari mara baada ya majadiliano, Ngeleja ambaye aligoma kutaja jina la kampuni iliyoteuliwa kuchunguza uhalali wa deni hilo ingawa alisema uchunguzi utakamilika kabla ya Juni mwaka huu, alisema masuala zaidi ya mgodi wa WDL yatajadiliwa katika kikao kijacho cha Bunge na kupewa ufumbuzi. “Kamati imeipongeza serikali kwa namna inavyoonyesha juhudi katika mchakato wa uuzwaji wa hisa na jinsi inavyorekebisha kasoro zilizopo na tunatumaini kabla ya Juni mwaka huu, taarifa kuhusu uhalali wa deni hilo itakuwa tayari,” alisema Ngeleja.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, hakuwa tayari kuzungumzia agizo alilopewa Ngeleja lakini alisema kamati imeishauri serikali kupitia wizara hiyo, kuangalia uwezekano wa kuuza hisa zake za asilimia 25 kwa wananchi. Katika hatua nyingine, habari za kuaminika kutoka katika kamati hiyo zilieleza kuwa leo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawasilisha ripoti ya Mpango Kazi wake lakini itakataliwa na kamati kutokana na kutowasilisha nyaraka katika kipindi cha siku saba iliyopewa.

Je, wewe una maoni yapi?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni

Nyuma Mbele