CCM huree Busanda
Saturday, 30 May, 2009, 12:15
Na Gazeti la Uhuru

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemtangaza mgombea ubunge wa jimbo la Busanda kwa tiketi ya CCM, Lolesia Bukwimba, kuwa mshindi baada ya kuwabwaga wapinzani wake watatu.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Daniel Mollel, alisema Lolesia amepata kura 29,242 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, mgombea wa CHADEMA, Finias Magessa, aliyepata kura 22,799.

Wagombea wengine walioshiriki katika uchaguzi huo ni Beatrice Lubambe wa UDP aliyepata kura 271 na mgombea wa CUF, Oscar Ndalahwa aliyepata kura 977.

Mollel kwa mujibu wa kifungu cha 81 A cha sheria ya uchaguzi, alimtangaza Lolesia baada ya kuwabwaga wapinzani wake hao.

"Kutokana na ushindi huu, namtangaza Lolesia Bukwimba wa CCM kuwa mshindi halali wa uchaguzi mdogo jimbo la BusandaÉendapo kuna mgombea mwenye malalamiko atapewa fomu kama ilivyo kawaida ili aweze kukata rufani," alisema Mollel.

Akizingumza muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Lolesia alisema anawashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua na kuwaahidi kuwa atafanya kazi kwa bidii.

"Nimeupokea ushindi huu kwa furaha na ninawashukuru wananchi wa Busanda kwa kunichagua, nawaahidi nitawatumikia wote," alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Hasna Mwilima, alimpongeza Lolesia kwa kuchaguliwa, ambapo pia alimshauri kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi zao kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyotaka.

"Nampongeza sana Lolesia kwa kuchaguliwa, pia namkumbusha kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao kama Ilani ya CCM inavyoelekeza," alisema Hasna.

Wananchi wa jimbo hilo nao walisema wameupokea ushindi wa Lolesia na CCM kwa jumla kwa furaha, ambapo pia waliwataka wagombea walioshindwa kujipanga kwa uchaguzi ujao.

Mwananchi ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini, alisema ushindi huo unaashiria CCM inazidi kukubalika nchini.

Uchaguzi huo ulitokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge, Faustine Rwilomba, Februari mwaka huu, akiwa kwenye matibabu nchini India.

Katika kampeni za uchaguzi wa Busanda, kila chama kilitumia mbinu zake, ambapo CHADEMA waliamua kutumia helikopta kwa nia ya kuibuka na ushindi.

Mbali ya kutumia helikopta, CHADEMA iliwahi kufanya operesheni maarufu kwa jina la sangara na ambayo matokeo ya uchaguzi yanaonyesha haikuwa na matunda yoyote ya maana.


[ 2 Ongeza Maoni ] ( 4 waliosoma mpaka sasa )   |  makala hii na maoni
Ikulu yawabana makatibu wakuu
Saturday, 30 May, 2009, 12:04

Na Mwananchi

BAADA ya kuwazuia wabunge kuwa wajumbe kwenye taasisi za kifedha, mianya ya ufisadi imezidi kubanwa baada ya Ikulu kuandaa waraka ambao utawaondoa makatibu wakuu wote katika nafasi za uenyekiti wa bodi za mashirika ya umma.

Katikati ya wiki, gavana wa Benki Kuu (BoT), alitoa maagizo kuwa taasisi za kifedha za umma hazitaruhusiwa kuwateua wabunge kuwa wajumbe wa bodi za taasisi hizo ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.

Kwa mujibu wa duru za habari za kuaminika, agizo la Ikulu limetolewa na katibu mkuu kiongozi, Philemon Luhanjo. Habari hizo zinasema hatua hiyo imefikiwa ili kuondoa mgongano wa kimaslahi katika utumishi wa umma.

Kaimu msajili wa hazina, Geoffrey Msella alikiri jana kuwa alipata taarifa za waraka huo, lakini akasema hajapata barua rasmi kutoka kwa katibu mkuu kiongozi.

"Nafikiri, inawezekana amewaandikia kwanza makatibu wakuu wenyewe na baadaye anaweza kuleta kwetu, lakini hadi sasa (jana) sijapata taarifa rasmi," alisema Msella.

Alipoulizwa kuhusu waraka huo, Luhanjo alisema hakuwa katika nafasi nzuri kuzungumza. "Siwezi kuzungumza kwa sasa nipo kwenye mkutano," alisema Luhanjo kwa kifupi jana jioni.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe alikiri kupata taarifa hizo alipohojiwa na Mwananchi, lakini akasema si rasmi bali amesikia.

Kutolewa kwa waraka huo wa kudhibiti watendaji hao wakuu wa wizara ni moja ya hatua kubwa za serikali katika kuimarisha utawala bora na kuondoa mgongano wa kimaslahi.

Baadhi ya makatibu wakuu ambao ni wenyeviti wa bodi za mshirika ya umma hadi sasa, ni pamoja na Bliandina Nyoni wa Wizara ya Afya. Kwa sasa, Nyoni ni mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF).

Mwingine ni Ramadhan Kijjah ambaye kwa sasa ni katibu mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi. Kijjah ni mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi wa Pesheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Jamii kwa Watumishi wa Serikali (PSPF).

Kwa mantiki hiyo, makatibu wakuu watabaki kuwa wajumbe wa bodi kutokana na mwingiliano wa shughuli za kiutendaji.

Una maoni yapi?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Wabunge waondolewa ulaji
Saturday, 30 May, 2009, 11:47
Na Habari Leo

Wabunge wameanza kunyang’anywa sehemu ya ulaji kutokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa waraka unaowaelekeza wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye bodi za mashirika na taasisi za fedha kuondolewa mara moja. Hatua hiyo inatokana na ushauri uliotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kushauri wabunge wasiwe wajumbe wa mashirika yoyote ya umma, ili kuondoa mgongano wa maslahi. Kaimu Msajili wa Hazina, Godfrey Sella, alisema jana kuwa utekelezaji wa waraka huo wa BoT unaanza mara moja. Alisema kuna baadhi ya wabunge wenye maslahi katika taasisi za kifedha; hivyo si vizuri viongozi hao kuwa sehemu ya bodi za wakurugenzi.

Tayari BoT imetoa orodha ya wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye taasisi za fedha na imepeleka waraka huo kwa Msajili wa Hazina ili aondoe majina ya wabunge hao kwenye bodi hizo. “Lengo hapa ni kutenganisha usimamizi na utekelezaji…tumepata waraka huo wa BoT na kinachofuata ni utekelezaji,” alisema Sella wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), aliyehoji sababu ya wabunge wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa mashirika ya umma wakati kuna baadhi yao wana uwezo.

Mbunge huyo alisema kama kuna chama cha siasa kimeshinikiza suala hilo ni vyema kikapuuzwa; kwa kile alichodai kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wabunge, kwani nao ni sehemu ya jamii. “Kuna wabunge wana uwezo mkubwa wa kuisaidia Serikali kupitia mashirika haya, iweje waondolewe kwenye nafasi zao za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma?” alihoji mbunge huyo. Baada ya swali hilo, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto, alifafanua kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kimekuwa kinashinikiza suala hilo; ila ni ushauri uliotolewa na ofisi ya CAG.

Ndipo Kaimu Msajili wa Hazina akafafanua, kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na akaeleza kuwa zina nia nzuri ya kuwafanya wabunge wawe wasimamizi wazuri wa mashirika hayo. Wakati huo huo, Msajili huyo wa Hazina alikiri kuwa kampuni za Meremeta na Buhemba hazijawasilisha hesabu zozote katika ofisi yake kwa kile alichodai kuwa wizara ndiyo yenye jukumu la kuomba hesabu hizo. Alisema Meremeta ambayo iko chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, haina hesabu zozote lakini pia BoT ambayo inahusika na kampuni hiyo nayo haina hesabu zake.

“Hii inahesabika kama ni kitegauchumi cha serikali, lakini kwa mtazamo wangu, si shirika la kitega uchumi kwani hata CAG ameshindwa kuifanyia ukaguzi, kwa vile haina mali inayoonekana kwa macho,” alisema Sella. Kuhusu majukumu ya ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Msajili huyo alilalamika kuwa ofisi yake imejikuta wakati mwingine ikifanya kazi za ndani za mashirika ya umma kutokana na mfumo wa kiutendaji uliopo. Alisema kwa sasa wanajitahidi kuandaa waraka utakaosaidia kufanya mabadiliko ili ofisi ya Msajili wa Hazina ibaki kuwa msimamizi wa mashirika ya umma bila kuingilia utendaji wa mashirika hayo.

“Tunataka sisi tubaki kusimamia na kuona kama uamuzi unaofanywa na mashirika haya unazingatia maslahi ya taifa,” alisema. Hata hivyo alisema kwa sasa wizara nyingi ambazo zinatakiwa zipeleke mapendekezo ya wajumbe wa bodi wa mashirika mbalimbali kabla ya kutangazwa, hazifanyi hivyo. Alisema licha ya sheria kuzitaka kufanya hivyo kwa makusudi, mawaziri wanakaidi. “Ukihoji utaulizwa Msajili ni nani na ukisema ufuate sheria lazima utagongana na wakubwa zako, ndiyo maana tunaamua kukaa kimya.”

Je, Una maoni yapi?

[ 1 Maoni ] ( 4 waliosoma mpaka sasa )   |  makala hii na maoni
Hisia za Uzanzibari, Utanganyika ndizo zitauzamisha Muungano
Thursday, 14 May, 2009, 16:24
Maoni ya Mhariri wa Nipashe

mekuwa kama ada, kila uchao kuna jambo jipya linajitokeza kama moja ya changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwelekeo wa siku za hivi karibuni unatoa picha kwamba Muungano wa nchi hizi mbili ni kama umejengwa juu ya urafiki wa kutokuaminiana.

Inawezekana uhuru wa kutoa maoni kwa njia za uwazi zaidi umetoa fursa kwa watu wengi zaidi kuzungumzia kasoro zilizoko katika Muungano wa huu, hali ambayo miaka kabla ya 90 haikuwako.



Tunaamini kwamba watu kuwa na uhuru wa kuzungumzia Muungano na changamoto zake ni njia moja sahihi ya kujenga; kwa maana kwamba kama udhaifu ukijulikana na kuzungumzwa basi watu watakuwa tayari kutatua hitilafu hizo. Wahenga walisema kujua tatizo ni nusu ya kupata utatuzi wake.



Pamoja na changamoto zote zinazoweza kutajwa kuwa ni kero hasa za Muungano, uamuzi wa hivi karibuni wa kuwataka Watanzania wenye asili ya Bara kulipa kodi ya ardhi ya Dola za Marekani 5,000 kwa mwaka sawa na raia wengine wa kigeni, hakika ni kielelezo kwamba wapo watu wanaochokonoa kadri wawezavyo ili kuudhoofisha Muungano!



Maamuzi haya yanadaiwa kuwa yanatokana na sheria ya ardhi ya mwaka 1992 ya Zanzibar ambayo inamtaja Mzanzibari pekee kuwa na haki ya kumiliki ardhi visiwani humo, wengine wote wanahesabika kama wageni, yaani hata Watanzania wanaotoka Bara wanatambuliwa kama wageni!



Kutokana na sheria hiyo, Watanzania kutoka Bara waliolowea na kujiendeleza Zanzibar kwa miaka, wakapata kipande cha ardhi na kuiendeleza sasa watalazimika kulipa kodi hiyo kwa mwaka kama walivyo wageni wengine wowote kutoka kona yoyote ya dunia hii.



Haya yakitokea Zanzibar, sheria za ardhi namba nne na tano za Tanzania za mwaka 1998, zinahalalisha kila Mtanzania kuwa na haki ya kumiliki ardhi. Mtanzania huyu aweza kuwa yule wa kuzaliwa au wa kuomba; wote wanaruhusiwa kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kigezo hiki kinawapa hata Wazanzibari haki ya kumiliki ardhi Bara.



Tunatambua kwamba wapo Wazanzibari wengi tu wajasiriamali waliobobea wamejiendeleza na sasa wanamiliki si tu ardhi, bali mali za uhakika zisizohamishika Tanzania Bara. Hawa wana haki kabisa mbele ya sheria kumiliki wanachomiliki na kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi, sisi tunawatia shime wawekeze zaidi na zaidi kwa ajili ya ustawi wa nchi yao.



Lakini wakati tukitambua sheria na hali halisi ya ardhi kwa pande zote za Muungano, yaani Zanzibar yenye ardhi finyu na Tanzania Bara yenye ardhi kubwa na fursa nyingi, tunapatwa na wasiwasi kwamba kwa nini katika kipindi hiki ambacho Muungano unapita katika kipindi cha majaribu makubwa, suala la kuwaweka kundi moja Watanzania wa Bara kundi moja na wageni linawekewa mkakati?



Tunashindwa kujua kama kweli msukumo pekee wa kuwaweka Watanganyika katika kundi la wageni visiwani Zanzibar ni matokeo ya mahitaji ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya visiwa hivyo, au ni njia nyingine ya mapambano kama nyingine nyingi ambazo zimeshuhudiwa katika siku za hivi za karibuni za Zanzibar kutaka kujionyesha kwamba ni taifa linalojitegemea?



Tunasema haya si kwa sababu tunaunga mkono mbinu zozote mbaya za kukandamiza haki za Wazanzibari, ila tunasukumwa na kitu kimoja; kwamba baada ya miaka 45 ya Muungano kila uchao tofauti zinatafutwa, kukuzwa na kupigiwa mbiu kana kwamba kufanya hivyo ndiyo njia ya kuujenga.



Tunapata hofu kwamba kama viongozi wetu wasipokaa kitako na kutafakari kwa mapana mambo yanayotengenezwa, kusukumwa na kupigiwa kampeni kuhusu udhaifu wa Muungano, kuna kila dalili kwamba huko tuendako mambo yatakuwa mabaya zaidi.



Tunafikiri huu si wakati wa kuendelea kubaguana baina ya Wazanzibari na Watanganyika, pia si wakati wa kuhoji nani ananufaika zaidi na kwa nini, ila kwa upeo wetu tunaamini huu ni wakati wa kushikamana zaidi, kuvuta kwa pamoja zaidi na kurekebisha kasoro zilizopo hata kama ni za kisheria ili kujenga Muungano imara zaidi. Tujitahidi kutibu kuliko kuendelea kubomoa.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Safari ni Ndefu: Baada ya Busanda ni Biharamulo!!!!
Thursday, 14 May, 2009, 10:21
Habari Leo (15.05.2009)

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mwingine mdogo katika Jimbo la Biharamulo Magharibi utakaofanyika Julai 5 mwaka huu. Uchaguzi huo ulitangazwa jana Dar es Salaam huku kampeni za vyama vya siasa zikiendelea wilayani Geita kwa ajili ya uchaguzi mwingine mdogo utakaofanyika mwezi huu jimboni Busanda.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu kwa waandishi wa habari, uteuzi wa wagombea utafanyika Juni 9 na kampeni zitaanzia Juni 10 hadi Julai 4 mwaka huu. Jimbo hilo lilikuwa wazi tangu Oktoba 12 mwaka juzi, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutengua matokeo ya uchaguzi na hivyo Mbunge aliyekuwapo kwa tikiti ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), Phares Kabuye kupoteza kiti chake.

Hata hivyo, Kabuye ambaye alifariki dunia mwezi uliopita, hakuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo alikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania. Wakati mchakato wa rufaa hiyo ulikuwa haujakamilika, Kabuye alikufa katika ajali ya basi mkoani Morogoro wakati akienda Dar es Salaam kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TLP.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema alisema chama chake kinajipanga kuhakikisha kinamweka mgombea makini atakayeendeleza historia ya kuongoza jimbo hilo.

Mrema aliviomba vyama vya upinzani kujenga umoja ili kukiwezesha chama chake kupata mwakilishi bungeni kwa kile alichoeleza kwamba TLP inafahamika na kukubalika kwa kiwango kikubwa jimboni humo. “TLP tulikuwa na katoto kamoja, kamekufa...tunaomba ushirikiano wa upinzani uanzie Biharamulo Magharibi kama hatua ya kumwenzi Kabuye,” alisema Mrema.

Je, Una maoni yapi?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Mambo ya Busanda
Thursday, 14 May, 2009, 10:12
Mwananchi 14.05.2009

Kampeni za uchaguzi wa ubunge Busanda zinazidi kuwa moto baada ya mkutano wa chama cha UDP kumalizika kwa watu kutawanyika huku wakimzomea Mwenyekiti wa chama hicho, John Momose Cheyo wakati akimtambulisha mgombea wao Beatrice Lubambe.

Mkutano huo ambao umefanyika katika eneo la Katoro jana ulimalizika kwa watu waliokuwa wamejaa wakimsilikiliza kusambaa huku wakipiga mayowe kumzomea alipoanza kumtambulisha mgombea wa chama chake.

Huo ni mkutano wa kwanza wa chama hicho tangu kuanza kwa kampeni hizo Aprili 29, mwaka huu.

Ilidaiwa kuwa UDP hawakuzindua kampeni zao rasmi kwa sababu ya kukabiliwa na ukata wa fedha.

Mkutano huo ambao ulianza na watu wachache, lakini baadaye waliongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele na kusikiliza kwa makini.

Hata hivyo mambo yaliharibika baada ya Cheyo kuanza kumwaga sera zake akisema wakimchagua mgombea wa UDP atateuliwa na kuwa mbunge ambapo atasimamia maendeleo ya eneo hilo pamoja na kuhakikisha kuwa bei ya pamba inapanda hadi kuwa Sh1,000 kwa kilo moja tofauti na bei ya sasa ya Sh 400.

“Nimezungumza kwa saa nzima mnanisikiliza sijatukana mtu, lakini wanasiasa wengine wanatukana hovyo hapa jukwaani, jambo hili haliwezi kufanya tulinde amani na uhuru wa kisiasa uliopo,” alieleza Cheyo.

Wakati huo wananchi walikuwa wametulia na kumsikiliza kwa makini, lakini alipomsimamisha mgombea wake walishika mikono kichwani na kumzomea kwa kupiga mayowe ya “uuwiiii”, huku wakitawanyika.

Kutokana na hatua hiyo Cheyo na mgombea wake walilazimika kuufunga mkutano wao na kuondoka haraka wakihofia kutokea vurugu.

[ 1 Maoni ] ( 7 waliosoma mpaka sasa )   |  makala hii na maoni
SMZ yazidi kuubomoa Muungano yataka bara walipe kodi ya ardhi
Sunday, 10 May, 2009, 10:41
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza mkakati mpya wa kuwataka wawekezaji na watu wenye asili ya Tanzania Bara kusajiliwa na kuanza kulipa kodi ya ardhi ya dola za Marekani 5000 (Sh6.5 milioni), kila mwaka kwa kila hekta moja ya ardhi.

Hata hivyo, SMZ ilisema mwekezaji mwenye asili ya Zanzibar atapaswa kulipa dola 500 (Sh650,000).

Mpango huo umetangazwa jana na Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mohammed Hashim Ismail kufuatia bodi hiyo kupewa uwakala wa kusimamia na kukusanya kodi ya ardhi.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Zanzibar ya mwaka 1992, Mzanzibari tu ndiye mwenye haki ya kumiliki ardhi, lakini wageni wote wanapaswa kukodishwa wakiwemo watu wenye asili ya Tanzania Bara.

“Hatua hii itatuwezesha pia kuwafahamu wamiliki wote wakubwa na wadogo wadogo wa vipande vyote vya ardhi hapa Zanzibar pamoja na wale ambao wanatajwa kuhodhi maeneo kinyume na utaratibu,” alisema kamishna huyo.

Alisema hatua hiyo itawasaidia kuwatambua wasiokuwa Wazanzibari na kuishauri serikali kuchukua hatua zinazofaa.

Kamishna huyo alisema viwango vya malipo vitapitiwa upya ili viende na wakati na kuishauri serikali juu ya hatua sinazostahili kuchukuliwa.

Alisema ardhi ni suala muhimu katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi wa Zanzibar, ndio maana serikali imeamua kuhakiki upya viwanja vya makazi kupitia mradi wa SMOLE.

Kamishna huyo alisema kupitia mradi huo taarifa zote zitaingizwa katika mfumo wa kompyuta ili kuweza kuwatambua watu wote waliokodishwa ardhi.

Hashim Ismail alisema kwamba bodi ya mapato imeanza kujitayarisha kwa ajili kukusanya fedha hizo pamoja na kuwatambua waliopewa ardhi kinyume cha sheria.

Hata hivyo zoezi hilo linatarajiwa kuibua mjadala mkubwa kutokana na ukweli kwamba, inachochea ubaguzi kati ya Watanzania Bara na Wazanzibari hivyo kuendelea kuudhoofisha muungano.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Pinda: Mishahara ya wabunge haitoshi
Thursday, 30 April, 2009, 13:18
Tanzania Daima 30.04.2009 (http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=4575)

WAKATI Bunge zima likimwandama Mbunge wa Karatu, Dk. Wilibrod Slaa (CHADEMA), kutokana na msimamo wake kuwa posho za wabunge ni kubwa na kutaka zipunguzwe, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameungana na wabunge wengine kwa kusema kuwa posho hizo ni ndogo na kutaka ziongezwe.

Ingawa hakutaja jina, lakini kauli hiyo ya Waziri Mkuu imeonekana dhahiri kumjibu Dk. Slaa anayetaka mishahara na posho za wabunge zipunguzwe, kwamba ni kubwa mno ukilinganisha na watumishi wengine wa umma.

Pinda aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua mpango mkakati wa Bunge wa miaka mitano, wenye nia ya kulifikisha Bunge katika kiwango cha juu cha ufanisi.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, Pinda alitumia mwanya huo kuchomeka suala la posho za wabunge, ambalo limekuwa agenda kubwa katika mkutano wa 15 wa Bunge unaomalizika leo.

Akielezea hatua ambazo serikali imekuwa ikizifanya kwa upande wa Bunge, Pinda ambaye aliorodhesha hatua kadhaa za kuboresha maslahi ya Bunge, alisema lengo la serikali ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa sasa bado ni ndogo.

“Lengo la serikali kwa Bunge ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa kweli kwa sasa hazifikii stahiki, lengo ni kuhakikisha Bunge linaboreshewa maslahi ili liweze kufanya kazi yake stahiki na kwa kiwango cha kuridhisha,” alisema Pinda.

Awali, akizungumzia malengo makubwa saba ya mpango mkakati huo, alisema moja ya malengo hayo ni kuboresha maslahi na stahiki za wabunge ili kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo.

Mbali na malengo hayo, mengine ya mkakati huo ni kuboresha muundo na utendaji wa ofisi za Bunge ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji, pia kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya sekretarieti ya Bunge.

Limo pia suala la kukuza na kuimarisha ushiriki wa Bunge kuwafikia wadau mbalimbali kupitia mikutano, machapisho, vyombo vya habari na njia nyingine ya mawasiliano, pamoja na kukuza na kuinua vipaji vya wabunge.

Kwa upande wa serikali, mbali na malengo ya kuboresha maslahi na posho za wabunge kwa kuzingatia mazingira ya utendaji wao wa kazi, na hali ya uchumi, Pinda pia aliyataja malengo mengine kuwa ni kuwezesha Bunge kuwa na ukumbi mzuri wa kisasa unaotosheleza mahitaji, lengo ambalo kwa sasa tayari limekwishatekelezwa.

Kwa mujibu wa Pinda, lengo lingine ni kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa Bunge ambao ulianza kutumika mwaka 2007/08, kuwashirikisha katika ziara za nje za viongozi wa kitaifa, lakini pia kuharakisha ujenzi wa ofisi za wabunge katika majimbo yao.

Tangu alipotoa kauli hiyo akiwa kwenye moja ya mikutano ya chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa akiandamwa na wabunge wenzake katika mkutano huu wa 15, wakipinga hoja hiyo kwa madai kuwa inawachonganisha wabunge na jamii.

Hali hiyo ilisababisha Dk. Slaa afikie hatua ya kuzomewa mara kadhaa kila jina lake linapotajwa kwenye vikao vya ndani na nje.

Mbunge huyo, hata hivyo, alisisitiza kwamba anasimama katika hoja zake, ikiwamo ya posho za wabunge kutaka kutazamwa upya.

Alisema ataendelea kuisimamia hoja hiyo kwa sababu anataka kuwapo kwa uwazi katika mishahara wanayolipwa viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge.


[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
TLP:Mutungirehi, Kinanda wapewa vyeo
Tuesday, 28 April, 2009, 07:24
Kutoka Magazetini

HALI imezidi kuwa tete ndani ya TLP, ambapo sasa kundi la wajumbe 750 wa mkutano mkuu wametangaza kutomtambua Mwenyekiti wa chama hicho Augustine Mrema, huku wakimtangaza Joram Kinanda kuwa Makamu Mwenyekiti na Benedicto Mutungirehi kuwa Katibu Mkuu wa TLP.

Hali hiyo imeibuka siku moja tu tangu chama hicho kilipofanya uchaguzi wake, uliomuweka Mrema madarakani. Hata hivyo, mizengwe, fitna na ubabe vinadaiwa kugubika uchaguzi huo, huku Mrema akituhumiwa kutumia ubabe kuwaengua wapinzani wake.

Mbali na wajumbe hao kutangaza kutomtambua Mrema, pia wamedai kuwa ni ‘fisadi papa’ wa kisiasa hivyo, hastahili kukiongoza chama hicho.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, jana, mwenyekiti wa kamati ya muda ya TLP, Macmillan Lyimo, alisema maamuzi hayo yamefikiwa na wajumbe, baada ya kufanya mkutano mkuu wa chama hicho katika ukumbi wa Millennium.

Alisema wajumbe hao zaidi ya 750 walinyimwa haki ya kikatiba kushiriki uchaguzi mkuu huo, ambao ulimuweka madarakani Mrema kinyume na utaratibu.

“Wajumbe waliomchagua Mrema na kumuweka madarakani ni wa halmashauri kuu, na si wajumbe wa mkutano mkuu…haiwezekani Mwenyekiti achaguliwe na wajumbe 120, ni kinyume na katiba ya chama, na lazima tumpeleka Mrema mahakamani,” alisema Lyimo.

Alisema, Katiba inatamka wajumbe 1,407 ndiyo wanaopaswa kushiriki uchaguzi, lakini alibadili katiba na kutangaza wajumbe waliotakiwa kuwa ni 163, na walioshiriki uchaguzi huo ni 123.

Kutokana na hatua hiyo, wajumbe hao chini ya Lyimo, walifanya uchaguzi wa kutafuta viongozi watakaoiongoza TLP, ambapo Kinanda aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na Mutungirehi kuwa Katibu Mkuu.

Katika uchaguzi uliofanyika juzi na kumuingiza madarakani kwa mara nyingine tena Mrema, wajumbe kutoka mikoa ya Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara, Kagera, Pwani hawakuhudhuria kikao hicho.

Gazeti hili lilipowasiliana na Mrema juu ya hali hiyo, alisema yeye ni mwenyekiti halali wa TLP, na kwamba hawatambui Mutungirehi na Kinanda.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Rais Kikwete atengua uteuzi wa DC wa Kishapu
Sunday, 26 April, 2009, 07:59
Na Mwananchi (25.04.2009)

RAIS Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wa Mkuu mpya wa Wilaya ya Kishapu, Anatory Choya muda mfupi baada ya kumtangaza na badala yake akamteua mwingine, Abdul Suleiman Lutavi.

Habari zilizopatikana zinaeleza kutenguliwa kwa uteuzi wa Choya ambaye ni mbunge wa zamani wa Biharamulo Magharibi mkoani Kagera, kutokana na kukamatwa na Takukuru na kufunguliwa kesi ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Biharamulo mwaka jana, nafasi ambayo alishinda.

Kesi yake namba 270 ya mwaka 2008 inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo na wiki iliyopita, Aprili 17 mwaka huu ilitajwa na inatarajiwa kutajwa tena Mei 11 mwaka huu.

Jumatatu wiki hii wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Shinyanga, pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwake walipigwa na butwaa baada ya kushuhudia akiapishwa Lutavi badala ya Choya.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dk Yohana Balele alimwapisha Lutavi na kuwafanya watu kuhoji kimya kimya nini kilichofanya Choya kushindwa kuapishwa na hakuna maelezo yaliyotolewa.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zinaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, alitengua uteuzi wa Choya kutokana na taarifa zilizoifikia ikulu kuwa Choya, anakabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani.

Hizi ni dalili nzuri. Je, wewe una maoni yapi ?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni

Mbele