Wabunge waondolewa ulaji
Saturday, 30 May, 2009, 11:47
Na Habari Leo

Wabunge wameanza kunyang’anywa sehemu ya ulaji kutokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa waraka unaowaelekeza wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye bodi za mashirika na taasisi za fedha kuondolewa mara moja. Hatua hiyo inatokana na ushauri uliotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kushauri wabunge wasiwe wajumbe wa mashirika yoyote ya umma, ili kuondoa mgongano wa maslahi. Kaimu Msajili wa Hazina, Godfrey Sella, alisema jana kuwa utekelezaji wa waraka huo wa BoT unaanza mara moja. Alisema kuna baadhi ya wabunge wenye maslahi katika taasisi za kifedha; hivyo si vizuri viongozi hao kuwa sehemu ya bodi za wakurugenzi.

Tayari BoT imetoa orodha ya wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye taasisi za fedha na imepeleka waraka huo kwa Msajili wa Hazina ili aondoe majina ya wabunge hao kwenye bodi hizo. “Lengo hapa ni kutenganisha usimamizi na utekelezaji…tumepata waraka huo wa BoT na kinachofuata ni utekelezaji,” alisema Sella wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), aliyehoji sababu ya wabunge wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa mashirika ya umma wakati kuna baadhi yao wana uwezo.

Mbunge huyo alisema kama kuna chama cha siasa kimeshinikiza suala hilo ni vyema kikapuuzwa; kwa kile alichodai kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wabunge, kwani nao ni sehemu ya jamii. “Kuna wabunge wana uwezo mkubwa wa kuisaidia Serikali kupitia mashirika haya, iweje waondolewe kwenye nafasi zao za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma?” alihoji mbunge huyo. Baada ya swali hilo, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto, alifafanua kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kimekuwa kinashinikiza suala hilo; ila ni ushauri uliotolewa na ofisi ya CAG.

Ndipo Kaimu Msajili wa Hazina akafafanua, kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na akaeleza kuwa zina nia nzuri ya kuwafanya wabunge wawe wasimamizi wazuri wa mashirika hayo. Wakati huo huo, Msajili huyo wa Hazina alikiri kuwa kampuni za Meremeta na Buhemba hazijawasilisha hesabu zozote katika ofisi yake kwa kile alichodai kuwa wizara ndiyo yenye jukumu la kuomba hesabu hizo. Alisema Meremeta ambayo iko chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, haina hesabu zozote lakini pia BoT ambayo inahusika na kampuni hiyo nayo haina hesabu zake.

“Hii inahesabika kama ni kitegauchumi cha serikali, lakini kwa mtazamo wangu, si shirika la kitega uchumi kwani hata CAG ameshindwa kuifanyia ukaguzi, kwa vile haina mali inayoonekana kwa macho,” alisema Sella. Kuhusu majukumu ya ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Msajili huyo alilalamika kuwa ofisi yake imejikuta wakati mwingine ikifanya kazi za ndani za mashirika ya umma kutokana na mfumo wa kiutendaji uliopo. Alisema kwa sasa wanajitahidi kuandaa waraka utakaosaidia kufanya mabadiliko ili ofisi ya Msajili wa Hazina ibaki kuwa msimamizi wa mashirika ya umma bila kuingilia utendaji wa mashirika hayo.

“Tunataka sisi tubaki kusimamia na kuona kama uamuzi unaofanywa na mashirika haya unazingatia maslahi ya taifa,” alisema. Hata hivyo alisema kwa sasa wizara nyingi ambazo zinatakiwa zipeleke mapendekezo ya wajumbe wa bodi wa mashirika mbalimbali kabla ya kutangazwa, hazifanyi hivyo. Alisema licha ya sheria kuzitaka kufanya hivyo kwa makusudi, mawaziri wanakaidi. “Ukihoji utaulizwa Msajili ni nani na ukisema ufuate sheria lazima utagongana na wakubwa zako, ndiyo maana tunaamua kukaa kimya.”

Je, Una maoni yapi?

[ 1 Maoni ] ( 4 waliosoma mpaka sasa )   |  makala hii na maoni
Hisia za Uzanzibari, Utanganyika ndizo zitauzamisha Muungano
Thursday, 14 May, 2009, 16:24
Maoni ya Mhariri wa Nipashe

mekuwa kama ada, kila uchao kuna jambo jipya linajitokeza kama moja ya changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwelekeo wa siku za hivi karibuni unatoa picha kwamba Muungano wa nchi hizi mbili ni kama umejengwa juu ya urafiki wa kutokuaminiana.

Inawezekana uhuru wa kutoa maoni kwa njia za uwazi zaidi umetoa fursa kwa watu wengi zaidi kuzungumzia kasoro zilizoko katika Muungano wa huu, hali ambayo miaka kabla ya 90 haikuwako.



Tunaamini kwamba watu kuwa na uhuru wa kuzungumzia Muungano na changamoto zake ni njia moja sahihi ya kujenga; kwa maana kwamba kama udhaifu ukijulikana na kuzungumzwa basi watu watakuwa tayari kutatua hitilafu hizo. Wahenga walisema kujua tatizo ni nusu ya kupata utatuzi wake.



Pamoja na changamoto zote zinazoweza kutajwa kuwa ni kero hasa za Muungano, uamuzi wa hivi karibuni wa kuwataka Watanzania wenye asili ya Bara kulipa kodi ya ardhi ya Dola za Marekani 5,000 kwa mwaka sawa na raia wengine wa kigeni, hakika ni kielelezo kwamba wapo watu wanaochokonoa kadri wawezavyo ili kuudhoofisha Muungano!



Maamuzi haya yanadaiwa kuwa yanatokana na sheria ya ardhi ya mwaka 1992 ya Zanzibar ambayo inamtaja Mzanzibari pekee kuwa na haki ya kumiliki ardhi visiwani humo, wengine wote wanahesabika kama wageni, yaani hata Watanzania wanaotoka Bara wanatambuliwa kama wageni!



Kutokana na sheria hiyo, Watanzania kutoka Bara waliolowea na kujiendeleza Zanzibar kwa miaka, wakapata kipande cha ardhi na kuiendeleza sasa watalazimika kulipa kodi hiyo kwa mwaka kama walivyo wageni wengine wowote kutoka kona yoyote ya dunia hii.



Haya yakitokea Zanzibar, sheria za ardhi namba nne na tano za Tanzania za mwaka 1998, zinahalalisha kila Mtanzania kuwa na haki ya kumiliki ardhi. Mtanzania huyu aweza kuwa yule wa kuzaliwa au wa kuomba; wote wanaruhusiwa kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kigezo hiki kinawapa hata Wazanzibari haki ya kumiliki ardhi Bara.



Tunatambua kwamba wapo Wazanzibari wengi tu wajasiriamali waliobobea wamejiendeleza na sasa wanamiliki si tu ardhi, bali mali za uhakika zisizohamishika Tanzania Bara. Hawa wana haki kabisa mbele ya sheria kumiliki wanachomiliki na kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi, sisi tunawatia shime wawekeze zaidi na zaidi kwa ajili ya ustawi wa nchi yao.



Lakini wakati tukitambua sheria na hali halisi ya ardhi kwa pande zote za Muungano, yaani Zanzibar yenye ardhi finyu na Tanzania Bara yenye ardhi kubwa na fursa nyingi, tunapatwa na wasiwasi kwamba kwa nini katika kipindi hiki ambacho Muungano unapita katika kipindi cha majaribu makubwa, suala la kuwaweka kundi moja Watanzania wa Bara kundi moja na wageni linawekewa mkakati?



Tunashindwa kujua kama kweli msukumo pekee wa kuwaweka Watanganyika katika kundi la wageni visiwani Zanzibar ni matokeo ya mahitaji ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya visiwa hivyo, au ni njia nyingine ya mapambano kama nyingine nyingi ambazo zimeshuhudiwa katika siku za hivi za karibuni za Zanzibar kutaka kujionyesha kwamba ni taifa linalojitegemea?



Tunasema haya si kwa sababu tunaunga mkono mbinu zozote mbaya za kukandamiza haki za Wazanzibari, ila tunasukumwa na kitu kimoja; kwamba baada ya miaka 45 ya Muungano kila uchao tofauti zinatafutwa, kukuzwa na kupigiwa mbiu kana kwamba kufanya hivyo ndiyo njia ya kuujenga.



Tunapata hofu kwamba kama viongozi wetu wasipokaa kitako na kutafakari kwa mapana mambo yanayotengenezwa, kusukumwa na kupigiwa kampeni kuhusu udhaifu wa Muungano, kuna kila dalili kwamba huko tuendako mambo yatakuwa mabaya zaidi.



Tunafikiri huu si wakati wa kuendelea kubaguana baina ya Wazanzibari na Watanganyika, pia si wakati wa kuhoji nani ananufaika zaidi na kwa nini, ila kwa upeo wetu tunaamini huu ni wakati wa kushikamana zaidi, kuvuta kwa pamoja zaidi na kurekebisha kasoro zilizopo hata kama ni za kisheria ili kujenga Muungano imara zaidi. Tujitahidi kutibu kuliko kuendelea kubomoa.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Safari ni Ndefu: Baada ya Busanda ni Biharamulo!!!!
Thursday, 14 May, 2009, 10:21
Habari Leo (15.05.2009)

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mwingine mdogo katika Jimbo la Biharamulo Magharibi utakaofanyika Julai 5 mwaka huu. Uchaguzi huo ulitangazwa jana Dar es Salaam huku kampeni za vyama vya siasa zikiendelea wilayani Geita kwa ajili ya uchaguzi mwingine mdogo utakaofanyika mwezi huu jimboni Busanda.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu kwa waandishi wa habari, uteuzi wa wagombea utafanyika Juni 9 na kampeni zitaanzia Juni 10 hadi Julai 4 mwaka huu. Jimbo hilo lilikuwa wazi tangu Oktoba 12 mwaka juzi, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutengua matokeo ya uchaguzi na hivyo Mbunge aliyekuwapo kwa tikiti ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), Phares Kabuye kupoteza kiti chake.

Hata hivyo, Kabuye ambaye alifariki dunia mwezi uliopita, hakuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo alikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania. Wakati mchakato wa rufaa hiyo ulikuwa haujakamilika, Kabuye alikufa katika ajali ya basi mkoani Morogoro wakati akienda Dar es Salaam kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TLP.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema alisema chama chake kinajipanga kuhakikisha kinamweka mgombea makini atakayeendeleza historia ya kuongoza jimbo hilo.

Mrema aliviomba vyama vya upinzani kujenga umoja ili kukiwezesha chama chake kupata mwakilishi bungeni kwa kile alichoeleza kwamba TLP inafahamika na kukubalika kwa kiwango kikubwa jimboni humo. “TLP tulikuwa na katoto kamoja, kamekufa...tunaomba ushirikiano wa upinzani uanzie Biharamulo Magharibi kama hatua ya kumwenzi Kabuye,” alisema Mrema.

Je, Una maoni yapi?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Mambo ya Busanda
Thursday, 14 May, 2009, 10:12
Mwananchi 14.05.2009

Kampeni za uchaguzi wa ubunge Busanda zinazidi kuwa moto baada ya mkutano wa chama cha UDP kumalizika kwa watu kutawanyika huku wakimzomea Mwenyekiti wa chama hicho, John Momose Cheyo wakati akimtambulisha mgombea wao Beatrice Lubambe.

Mkutano huo ambao umefanyika katika eneo la Katoro jana ulimalizika kwa watu waliokuwa wamejaa wakimsilikiliza kusambaa huku wakipiga mayowe kumzomea alipoanza kumtambulisha mgombea wa chama chake.

Huo ni mkutano wa kwanza wa chama hicho tangu kuanza kwa kampeni hizo Aprili 29, mwaka huu.

Ilidaiwa kuwa UDP hawakuzindua kampeni zao rasmi kwa sababu ya kukabiliwa na ukata wa fedha.

Mkutano huo ambao ulianza na watu wachache, lakini baadaye waliongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele na kusikiliza kwa makini.

Hata hivyo mambo yaliharibika baada ya Cheyo kuanza kumwaga sera zake akisema wakimchagua mgombea wa UDP atateuliwa na kuwa mbunge ambapo atasimamia maendeleo ya eneo hilo pamoja na kuhakikisha kuwa bei ya pamba inapanda hadi kuwa Sh1,000 kwa kilo moja tofauti na bei ya sasa ya Sh 400.

“Nimezungumza kwa saa nzima mnanisikiliza sijatukana mtu, lakini wanasiasa wengine wanatukana hovyo hapa jukwaani, jambo hili haliwezi kufanya tulinde amani na uhuru wa kisiasa uliopo,” alieleza Cheyo.

Wakati huo wananchi walikuwa wametulia na kumsikiliza kwa makini, lakini alipomsimamisha mgombea wake walishika mikono kichwani na kumzomea kwa kupiga mayowe ya “uuwiiii”, huku wakitawanyika.

Kutokana na hatua hiyo Cheyo na mgombea wake walilazimika kuufunga mkutano wao na kuondoka haraka wakihofia kutokea vurugu.

[ 1 Maoni ] ( 7 waliosoma mpaka sasa )   |  makala hii na maoni
SMZ yazidi kuubomoa Muungano yataka bara walipe kodi ya ardhi
Sunday, 10 May, 2009, 10:41
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza mkakati mpya wa kuwataka wawekezaji na watu wenye asili ya Tanzania Bara kusajiliwa na kuanza kulipa kodi ya ardhi ya dola za Marekani 5000 (Sh6.5 milioni), kila mwaka kwa kila hekta moja ya ardhi.

Hata hivyo, SMZ ilisema mwekezaji mwenye asili ya Zanzibar atapaswa kulipa dola 500 (Sh650,000).

Mpango huo umetangazwa jana na Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mohammed Hashim Ismail kufuatia bodi hiyo kupewa uwakala wa kusimamia na kukusanya kodi ya ardhi.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Zanzibar ya mwaka 1992, Mzanzibari tu ndiye mwenye haki ya kumiliki ardhi, lakini wageni wote wanapaswa kukodishwa wakiwemo watu wenye asili ya Tanzania Bara.

“Hatua hii itatuwezesha pia kuwafahamu wamiliki wote wakubwa na wadogo wadogo wa vipande vyote vya ardhi hapa Zanzibar pamoja na wale ambao wanatajwa kuhodhi maeneo kinyume na utaratibu,” alisema kamishna huyo.

Alisema hatua hiyo itawasaidia kuwatambua wasiokuwa Wazanzibari na kuishauri serikali kuchukua hatua zinazofaa.

Kamishna huyo alisema viwango vya malipo vitapitiwa upya ili viende na wakati na kuishauri serikali juu ya hatua sinazostahili kuchukuliwa.

Alisema ardhi ni suala muhimu katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi wa Zanzibar, ndio maana serikali imeamua kuhakiki upya viwanja vya makazi kupitia mradi wa SMOLE.

Kamishna huyo alisema kupitia mradi huo taarifa zote zitaingizwa katika mfumo wa kompyuta ili kuweza kuwatambua watu wote waliokodishwa ardhi.

Hashim Ismail alisema kwamba bodi ya mapato imeanza kujitayarisha kwa ajili kukusanya fedha hizo pamoja na kuwatambua waliopewa ardhi kinyume cha sheria.

Hata hivyo zoezi hilo linatarajiwa kuibua mjadala mkubwa kutokana na ukweli kwamba, inachochea ubaguzi kati ya Watanzania Bara na Wazanzibari hivyo kuendelea kuudhoofisha muungano.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Pinda: Mishahara ya wabunge haitoshi
Thursday, 30 April, 2009, 13:18
Tanzania Daima 30.04.2009 (http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=4575)

WAKATI Bunge zima likimwandama Mbunge wa Karatu, Dk. Wilibrod Slaa (CHADEMA), kutokana na msimamo wake kuwa posho za wabunge ni kubwa na kutaka zipunguzwe, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameungana na wabunge wengine kwa kusema kuwa posho hizo ni ndogo na kutaka ziongezwe.

Ingawa hakutaja jina, lakini kauli hiyo ya Waziri Mkuu imeonekana dhahiri kumjibu Dk. Slaa anayetaka mishahara na posho za wabunge zipunguzwe, kwamba ni kubwa mno ukilinganisha na watumishi wengine wa umma.

Pinda aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akizindua mpango mkakati wa Bunge wa miaka mitano, wenye nia ya kulifikisha Bunge katika kiwango cha juu cha ufanisi.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, Pinda alitumia mwanya huo kuchomeka suala la posho za wabunge, ambalo limekuwa agenda kubwa katika mkutano wa 15 wa Bunge unaomalizika leo.

Akielezea hatua ambazo serikali imekuwa ikizifanya kwa upande wa Bunge, Pinda ambaye aliorodhesha hatua kadhaa za kuboresha maslahi ya Bunge, alisema lengo la serikali ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa sasa bado ni ndogo.

“Lengo la serikali kwa Bunge ni kuboresha maslahi na posho za wabunge ambazo kwa kweli kwa sasa hazifikii stahiki, lengo ni kuhakikisha Bunge linaboreshewa maslahi ili liweze kufanya kazi yake stahiki na kwa kiwango cha kuridhisha,” alisema Pinda.

Awali, akizungumzia malengo makubwa saba ya mpango mkakati huo, alisema moja ya malengo hayo ni kuboresha maslahi na stahiki za wabunge ili kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo.

Mbali na malengo hayo, mengine ya mkakati huo ni kuboresha muundo na utendaji wa ofisi za Bunge ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji, pia kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya sekretarieti ya Bunge.

Limo pia suala la kukuza na kuimarisha ushiriki wa Bunge kuwafikia wadau mbalimbali kupitia mikutano, machapisho, vyombo vya habari na njia nyingine ya mawasiliano, pamoja na kukuza na kuinua vipaji vya wabunge.

Kwa upande wa serikali, mbali na malengo ya kuboresha maslahi na posho za wabunge kwa kuzingatia mazingira ya utendaji wao wa kazi, na hali ya uchumi, Pinda pia aliyataja malengo mengine kuwa ni kuwezesha Bunge kuwa na ukumbi mzuri wa kisasa unaotosheleza mahitaji, lengo ambalo kwa sasa tayari limekwishatekelezwa.

Kwa mujibu wa Pinda, lengo lingine ni kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa Bunge ambao ulianza kutumika mwaka 2007/08, kuwashirikisha katika ziara za nje za viongozi wa kitaifa, lakini pia kuharakisha ujenzi wa ofisi za wabunge katika majimbo yao.

Tangu alipotoa kauli hiyo akiwa kwenye moja ya mikutano ya chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa akiandamwa na wabunge wenzake katika mkutano huu wa 15, wakipinga hoja hiyo kwa madai kuwa inawachonganisha wabunge na jamii.

Hali hiyo ilisababisha Dk. Slaa afikie hatua ya kuzomewa mara kadhaa kila jina lake linapotajwa kwenye vikao vya ndani na nje.

Mbunge huyo, hata hivyo, alisisitiza kwamba anasimama katika hoja zake, ikiwamo ya posho za wabunge kutaka kutazamwa upya.

Alisema ataendelea kuisimamia hoja hiyo kwa sababu anataka kuwapo kwa uwazi katika mishahara wanayolipwa viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge.


[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
TLP:Mutungirehi, Kinanda wapewa vyeo
Tuesday, 28 April, 2009, 07:24
Kutoka Magazetini

HALI imezidi kuwa tete ndani ya TLP, ambapo sasa kundi la wajumbe 750 wa mkutano mkuu wametangaza kutomtambua Mwenyekiti wa chama hicho Augustine Mrema, huku wakimtangaza Joram Kinanda kuwa Makamu Mwenyekiti na Benedicto Mutungirehi kuwa Katibu Mkuu wa TLP.

Hali hiyo imeibuka siku moja tu tangu chama hicho kilipofanya uchaguzi wake, uliomuweka Mrema madarakani. Hata hivyo, mizengwe, fitna na ubabe vinadaiwa kugubika uchaguzi huo, huku Mrema akituhumiwa kutumia ubabe kuwaengua wapinzani wake.

Mbali na wajumbe hao kutangaza kutomtambua Mrema, pia wamedai kuwa ni ‘fisadi papa’ wa kisiasa hivyo, hastahili kukiongoza chama hicho.

Akizungumza mjini Dar es Salaam, jana, mwenyekiti wa kamati ya muda ya TLP, Macmillan Lyimo, alisema maamuzi hayo yamefikiwa na wajumbe, baada ya kufanya mkutano mkuu wa chama hicho katika ukumbi wa Millennium.

Alisema wajumbe hao zaidi ya 750 walinyimwa haki ya kikatiba kushiriki uchaguzi mkuu huo, ambao ulimuweka madarakani Mrema kinyume na utaratibu.

“Wajumbe waliomchagua Mrema na kumuweka madarakani ni wa halmashauri kuu, na si wajumbe wa mkutano mkuu…haiwezekani Mwenyekiti achaguliwe na wajumbe 120, ni kinyume na katiba ya chama, na lazima tumpeleka Mrema mahakamani,” alisema Lyimo.

Alisema, Katiba inatamka wajumbe 1,407 ndiyo wanaopaswa kushiriki uchaguzi, lakini alibadili katiba na kutangaza wajumbe waliotakiwa kuwa ni 163, na walioshiriki uchaguzi huo ni 123.

Kutokana na hatua hiyo, wajumbe hao chini ya Lyimo, walifanya uchaguzi wa kutafuta viongozi watakaoiongoza TLP, ambapo Kinanda aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na Mutungirehi kuwa Katibu Mkuu.

Katika uchaguzi uliofanyika juzi na kumuingiza madarakani kwa mara nyingine tena Mrema, wajumbe kutoka mikoa ya Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara, Kagera, Pwani hawakuhudhuria kikao hicho.

Gazeti hili lilipowasiliana na Mrema juu ya hali hiyo, alisema yeye ni mwenyekiti halali wa TLP, na kwamba hawatambui Mutungirehi na Kinanda.

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Rais Kikwete atengua uteuzi wa DC wa Kishapu
Sunday, 26 April, 2009, 07:59
Na Mwananchi (25.04.2009)

RAIS Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wa Mkuu mpya wa Wilaya ya Kishapu, Anatory Choya muda mfupi baada ya kumtangaza na badala yake akamteua mwingine, Abdul Suleiman Lutavi.

Habari zilizopatikana zinaeleza kutenguliwa kwa uteuzi wa Choya ambaye ni mbunge wa zamani wa Biharamulo Magharibi mkoani Kagera, kutokana na kukamatwa na Takukuru na kufunguliwa kesi ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Biharamulo mwaka jana, nafasi ambayo alishinda.

Kesi yake namba 270 ya mwaka 2008 inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo na wiki iliyopita, Aprili 17 mwaka huu ilitajwa na inatarajiwa kutajwa tena Mei 11 mwaka huu.

Jumatatu wiki hii wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Shinyanga, pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwake walipigwa na butwaa baada ya kushuhudia akiapishwa Lutavi badala ya Choya.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Brigedia Jenerali Dk Yohana Balele alimwapisha Lutavi na kuwafanya watu kuhoji kimya kimya nini kilichofanya Choya kushindwa kuapishwa na hakuna maelezo yaliyotolewa.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zinaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete, alitengua uteuzi wa Choya kutokana na taarifa zilizoifikia ikulu kuwa Choya, anakabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani.

Hizi ni dalili nzuri. Je, wewe una maoni yapi ?

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Mfanyabiashara maarufu Reginald Mengi ajitoa mhanga kwa mafisadi
Saturday, 25 April, 2009, 10:17
Na Mwananchi 23.04.2009

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Reginald Mengi jana aliamua kujitoa muhanga alipotangaza majina ya wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia ambao anadai kuwa ni mafisadi papa wanaoiba mabilioni ya fedha za wananchi na kutaka wachukuliwe hatua kwa madai kuwa wataiyumbisha na kuitingisha nchi.

Kati ya wafanyabiashara waliotajwa na Mengi, wawili wamefunguliwa mashtaka ya tuhuma za wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), wengine wakiwa wameshatajwa kwenye kashfa mbalimbali, zikiwemo za zabuni ya utoaji umeme wa dharura ya Richmond Development na uuzwaji wa jengo la Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mengi, ambaye anamiliki kampuni ya IPP yenye kampuni mbalimbali zikiwemo za habari na vinywaji, alitaja wafanyabiashara hao watano akisema kuwa ndio papa kwa ufisadi lakini akasema idadi ya mafisadi wanaofilisi nchi hawazidi 10.

"Wanaotuhumiwa kuwa mafisadi papa wanahusishwa na karibu kila kashfa kubwa hapa nchini zikiwepo kashfa za Richmond, EPA, Dowans, helikopta na magari ya jeshi, ndege ya rais, rada, NSSF, Bahati Nasibu ya Taifa, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na kadhalika," alidai Mengi katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya kwenye ofisi yake jijini Dar es salaam.

Kati ya wafanyabiashara hao watano ambao Mengi alidai ni mapapa wa ufisadi, wamo Rostam Aziz, Yusuf Manji na Jayantkumar Chandubhai Patel (Jeetu Patel), ambao Mwananchi ilipata nafasi ya kuzungumza nao kuhusu tuhuma hizo za Mengi.

Hata hivyo, Mengi hakuwa tayari kutoa vielelezo kuthibitisha madai yake, lakini akasema iwapo watamshtaki mahakamani na wafanye hivyo kwa kuwa huko ndiko haki inakopatikana.

Mengi alirusha tuhuma nyingi kwa watu hao ambao alidai kuwa wamecharuka baada ya Rais Jakaya Kikwete kuamua kupambana nao na hivyo wameamua kupambana na yeyote anayemsaidia mkuu huyo wa nchi katika vita hiyo.

"Jitihada kubwa za Mhe. Rais za kuleta maendeleo na maisha bora kwa kila Mtanzania zinazoofishwa na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa. Bado Watanzania wengi wanaandamwa na umaskini mkubwa; hawajui hata mlo mmoja kwa siku utatoka wapi," alidai Mengi ambaye pia alitoa taarifa ya maandishi aliyoisaini.

"Cha kusikitisha ni kuwa pale Mtanzania mwema mwenye uwezo anaposaidia jamii kuondokana na umasikini, mafisadi wanapiga kelele kuwa misaada ya aina hiyo ina agenda. Wanapinga kwa kuwa wanataka Watanzania wafe na njaa na matatizo mengine."

Mengi alikwenda mbali zaidi na kudai mafisadi anaowatuhumu wanaweza wakaunga mkono matatizo yanayotokana na Deci, taasisi inayoendesha mchezo wa kuchangisha fedha na kulipa maradufu na Watanzania kubakia "wakifukuzana na wachungaji bila ya kujiuliza ni kina nani hasa wanachochea vurugu".

Wakiongea na Mwananchi, watu hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi hawakutaka kujibu kwa kirefu na badala yake walimtuhumu mwenyekiti huyo mtendaji wa IPP kuwa ana wivu, fitina chuki na ambaye ameshindwa kuendesha nyumba na biashara zake, huku mwingine akieleza kuwa anatumia haki yake ya kidemokrasia ya kutoa maoni yake.

"Mengi... (si mstaarabu)," alisema Manji ambaye anamiliki kampuni ya Quality Group. " Biashara zake zimemshinda ndio maana anazungumza ovyo."

Rostam Aziz, ambaye ni mbunge wa Igunga anayejishughulisha na biashara mbalimbali za miradi mikubwa ya ujenzi, uchimbaji na habari, alimuelezea Mengi kama mtu ambaye analingana kwa umri na baba yake mzazi na hivyo hawezi kubishana naye.

Lakini akasema: "Mengi amejaa chuki, wivu na fitina. Sina cha kumsaidia isipokuwa kumuombea Mungu ili amsaidie kwa kumpuuzia hayo maana ni adhabu kwa nafsi yake mwenyewe. Kwa malezi niliyopata, siwezi kubishana na mzee."

Jeetu Patel naye alisema haoni busara kujibizana na Mengi na kwamba alichofanya mwenyekiti huyo wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda (CTI) ni kutumia haki yake ya kidemokrasia ya uhuru wa kuongea.

“Hayo ni matatizo yake," alisema Patel, ambaye anakabiliwa na kesi ya tuhuma za wizi wa fedha za EPA. "Amewaita waandishi kuzungumza nao... sikumsikia lakini ninachoweza kusema ni kwamba anatumia uhuru wake wa kujieleza.

"Binafsi sijui chochote kuhusu hizo tuhuma za Mengi dhidi yangu, ila anayo haki ya kusema chochote. Nina mambo mengi ya kufanya hivyo sioni kama itanisaidia kwenye biashara zangu za kila siku kuanza majibizano na Mengi."

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mengi alidai kuwa watu hao aliowataja si tu kwamba wanaiba rasilimali za Tanzania, bali pia wanaiba muda wa Watanzania.

"Badala ya kutumia muda katika shughuli za maendeleo, tunajikuta tukitumia muda mwingi kupambana nao na hawatingishiki," alidai Mengi. "Badala yake wanatumia fedha walizotuibia kuanzisha magazeti ya kujenga kiburi cha kutudharau, kututukana na kutunyanyasa. Inakuwa kesi ya mwizi kumkimbiza na kumpiga aliyeibiwa.

"Hata sasa hivi, mafisadi papa wanaendelea kutumia uwezo wao wa kiuchumi uliotokana na wizi wa rasilimali za nchi yetu kushawishi na kupata miradi mikubwa mikubwa kwa kutumia majina tofauti tofauti huku wakipuuza kabisa kelele za wananchi kuhusu ufisadi wao.

Alisema ni muhimu wananchi wakajiuliza hawa mafisadi wanapata wapi ujasiri wa majigambo, dharau na nguvu za kutukana na kunyanyasa watu.

Alisema mafisadi papa ni lazima wajue kwamba iwapo wapambanaji wa ufisadi watapata madhara kwa njia yoyote hapa nchini au nje ya nchi, wananchi wa Tanzania watawawajibisha.

"Ni lazima Watanzania wote tuone kwamba sasa tumefika mahali pa kusema imetosha," alidai Mengi.


[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni
Dk. Slaa azomewa bungeni
Saturday, 25 April, 2009, 09:58
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, jana alilazimika kuwasihi na kuwaomba wabunge kuwa watulivu, baada ya ukumbi kulipuka wakimzomea Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA).

Kizaazaa hicho kilianza baada ya Spika Sitta kutangaza kuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Dk. Slaa alikuwa ameomba kukutana na wajumbe wa kamati hiyo jana saa tano asubuhi.

Kutajwa kwa jina la Dk. Slaa kulizusha kelele za kumzomea mbunge huyo, jambo lililomfanya Spika kushindwa kuendelea na matangazo ya shughuli za asubuhi.

“Waheshimiwa wabunge naomba utulivu, najua misimamo ya Dk. Slaa imesimama katika upotoshaji, lakini yeye (Dk. Slaa) ni mwenyekiti wa kamati na ana haki ya kuitisha vikao,” alisema Spika Sitta.

Dk. Slaa amekuwa akishutumiwa na wabunge wenzake kutokana na msimamo wake kwamba, wabunge wanalipwa mshahara mkubwa ikilinganishwa na mishahara ya wafanyakazi wengine wa kawaida.

Msimamo huo wa Dk. Slaa umepingwa na wabunge wengi, wakiwemo wa upinzani wakidai kitendo chake cha kusimama kwenye majukwaa ya siasa na kutangaza mshahara wa wabunge ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Baadhi ya wabunge walipendekeza Dk. Slaa kutokana na kitendo chake cha kuwachonganisha wabunge na wananchi, aondolewe katika nafasi ya mwenyekiti wa kamati hiyo.

Juzi iliripotiwa kwamba, Dk. Slaa alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge, wakiwemo kutoka kambi ya upinzani kumshambulia kutokana na kutangaza mshahara na marupurupu ya ubunge kwa wapiga kura wake.

Imeelezwa kuwa hilo lilijitokeza katika kikao cha ndani cha wabunge, kilichofanyika baada ya kipindi cha maswali na majibu, ambapo walisema kitendo cha Dk. Slaa ni ukiukwaji wa maadili ya Bunge.

Miongoni mwa wabunge waliomvaa Dk. Slaa ni Lucas Selelii (Nzega-CCM), aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Bunge kutokana na kitendo hicho cha ukiukwaji wa maadili.

Mwingine ni John Cheyo (Bariadi Mashariki -UDP), aliyemweleza Dk. Slaa kwamba urais haupatikani kwa njia anazotumia.

Naye Anna Komu (Viti Maalumu-CHADEMA) alisema anashangazwa na ukimya wa Bunge baada ya Dk. Slaa kutoa kauli hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati wabunge wakimshambulia, Dk. Slaa alikuwa kimya.

Je, ni halali kumzomea? Pili je mishahara minono kwa wabunge tu ndiyo uwakilishi? Jadili

[ Weka Maoni ]   |  makala hii na maoni

Mbele