Kutoka Magazeti ya GP: HONGERA CCM KUWADHIBITI WANACHAMA WAROPOKAJI
Thursday, 20 August, 2009, 06:52
watu wenyewe binafsi na si sera au mfumo wa CCM ambao unajulikana kabisa katika kupiga vita uovu wowote ndani ya chama na katika jamii ambayo inaongozwa na serikali yake.
Kwa kifupi, wanachama hao wamekuwa wakinyea kwenye mkeka ambao wanaulalia na ambao wataendelea kuulalia!
Katika mazingira ya sasa ambayo ni ya ushindani wa kisiasa, ni bora wanachama wa CCM wakatambua mfumo uliopo unaotumiwa katika kukosoana miongoni mwa wanachama wake. Na watambue kwamba katika mfumo wa vyama vingi, siasa imekuwa sawa na soko huria. Soko huria kwa maana kwamba vyama vina sera zake na namna ya kuendesha si mapambano yake tu bali na namna ya kujihami.
Hivyo, Wabunge wa CCM na wanachama wengine ambao wamekuwa wakiiyumbisha serikali yao kwa makusudi au bila kujua, wafahamu wamekuwa wakifanya hivyo kwa faida ya vyama vya upinzani na kwa hasara ya CCM!
Tabia ya kusema hadharani kauli zenye kukivunjia hadhi chama chao – badala ya vikao husika vyenye lengo la kukosoana na kuwekana sawa – ni ukiukaji wa kanuni zinazoongoza nidhamu ya chama, hulka ambayo ikiachwa kuendelea, itakiangamiza chama.
Ikumbukwe kwamba CCM ndicho kilichowafikisha mahali walipo watu ambao wanakishambulia kutoka ndani yake. Na pia lazima wafahamu kwamba hakuna chama au kikundi chochote ambacho wanachama wake hawana dhambi au madhambi yoyote!
Pia ni muhimu kufahamu kwamba chama ni kama familia moja ambayo ina kiongozi wake na mfumo maalum wa kutatua matatizo yake.
Ni tabia mbaya ndugu wa familia moja kusaidia kufichua siri au matatizo ya ndani ya familia, hata kama watu wa nje tayari wanayaelewa. Kufanya hivyo, ni kuidhalilisha zaidi familia, na anayefanya hivyo lazima afahamu anajidhalilisha na yeye pia kwani ni lazima atakuwa ameshiriki kwa namna fulani katika kuibuka kwa matatizo ya familia hiyo.
Na dawa ya kumaliza matatizo ya ndani ya familia, ni kwa familia yenyewe kukaa na kuyajadili na kuyapatia mwafaka badala ya kuwasaidia watu wa nje kuyafahamu zaidi, kwani maadui zao wanaweza kuyatumia kuifarakanisha zaidi familia hiyo.
Kwa kweli, kitendo cha kuwaunga mkono wapinzani katika kukipiga vita Chama Cha Mapinduzi ni usaliti wa wazi wa kutoa siri za matatizo ya familia kwa watu wa nje.
Kitu muhimu kwa kila mwanachama wa CCM ni kufahamu kwamba kutoa siri yoyote ya ndani na kuipeleka mitaani ni jambo la madhara makubwa kwani likikosa ufumbuzi kwa kuzidiwa na fedheha matokeo yake ni kufarakanika kwa familia.
Jambo la kuzingatia ni kwamba kama kweli wanachama wa CCM wanaamini kwamba kuyatoa matatizo ya ndani na kuyapeleka mitaani ndiyo ufumbuzi wa matatizo hayo, ni bora wakajiunga na vyama vya upinzani ambavyo vimeyashikilia bango matatizo binafsi ya baadhi ya wanachama wa CCM.
Na ni vyema wakafanya hivyo mapema!
Je, wewe una maoni yapi?
[ Weka Maoni ] | makala hii na maoni
Wananchi wachoma nyumba na kuharibu shamba la mbunge
Tuesday, 9 June, 2009, 13:12
Na Mwanachi
MAMIA ya wakazi wa kijiji cha Sing'isi kilicho wilayani Arumeru mkoani Arusha, wamevamia kwa siku mbili mfululizo shamba la Madira Estate linalomilikiwa na Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro na kuteketeza kwa moto zaidi ya nyumba 15 zilizo kuwa kwenye shamba hilo na kukata mazao kadhaa yenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Tukio hili limetokea wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa mjini hapa kushiriki matembezi ya kuchangia mradi wa kutoa chakula mashuleni yaliyoandaliwa na Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Wananchi hao waliokuwa na mapanga, visu, nondo na silaha nyingine kadhaa, walianza uvamizi wa shamba hilo kuanzia majira ya saa 3:00 usiku juzi na kuendelea hadi jana asubuhi, vitendo vilivyosababisha kufungwa kwa muda barabara ya Arusha-Moshi.
Licha ya polisi kumwagwa katika eneo hilo na kupiga mabomu kadhaa ya machozi na risasi kadhaa za moto hewani, wananchi hao waliendelea na uharibifu huo na kubeba mbao, mabati na mali mbalimbali zilizokuwa katika eneo hilo.
Wakizungumza katika eneo hilo, baadhi ya wananchi walisema wanapinga serikali kuliuza shamba hilo lenye ekari 50 kwa mbunge huyo wakati wao wana shida kubwa ya ardhi na eneo la upanuzi wa shule yao.
'Hatukubali... hili ni eneo letu. Tutapigana hadi mwisho na hakuna kumilikiwa tena na mbunge. Tumefunga barabara na tumevunja nyumba zote... serikali ilipaswa kutupa eneo letu wananchi baada ya Wazungu kuacha mashamba, lakini ajabu imeliuza," alisema John Akyo mkazi wa kijiji hicho.
Mkuu wa wilaya hiyo, Marcy Silla aliyefika eneo hilo jana asubuhi, alionekana kupigwa na butwaa wakati akishuhudia ujasiri wa wananchi kuendelea kubeba mali mbalimbali kutoka katika nyumba zaidi ya 15 walizovunja, nyumba ambazo zipo ndani ya shamba na nyingine ambazo mbunge huyo amezirithi.
"Sijui lolote kuhusu tukio hili. Nimepewa taarifa leo, lakini nilichoelezwa ni kwamba wananchi wanadai eneo, lakini kweli kwa nini watumie nguvu kiasi hiki," alihoji Silla.
Kimaro, akizungumza na mwandishi wa habari jana, alisema ameshangazwa na uamuzi wa wananchi kuvamia eneo lake pekee wakati jirani kuna Wazungu wana zaidi ya ekari 1,000.
"Nilipata taarifa hizi tangu juzi, nikawapa taarifa polisi, lakini nashangaa hawajachukua hatua hadi usiku wananchi walipovamia shamba. Mimi mzalendo mwenzao kumiliki heka 50 kujenga hoteli imekuwa nongwa!" alisema Kimaro.
Alisema anaamini tukio hilo sio shamba tu, bali kuna siasa ndani yake kwa kuwa anataka kujenga hoteli na ndio maana alianza kulitunza eneo kwa kupanda miti ya asili ambayo imekatwa na wananchi hao.
"Kuna miti zaidi ya 4,000 imekatwa na wananchi. Wanasema eti wanataka kulima... lile eneo ni la hoteli ya kitalii na kabla ya ujenzi nilikuwa nalirejesha kwenye uasilia wake," alisema Kimaro.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Matei Basilio alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba hadi jana zaidi ya watu 15 walikuwa wamekamatwa.
"Ni kweli kuna vurugu tangu usiku na vijana wangu wanashughulikia na hadi sasa watu wanakamatwa na vurugu zinaendelea," alisema Basilio jana mchana.
Diwani wa kata hiyo, Petro Kiungani na mwenyekiti wa kitongoji cha Maviruni yalipo mashamba hayo, Desaulo Akyoo, walisema kwa zaidi ya wiki wamekuwa wakitoa taarifa polisi juu ya mpango huo wa uvamizi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
"Nilimweleza mkuu wa polisi wa wilaya kuna vikao vinaitishwa kuchochea vurugu. Wananchi walikuwa wakidai sisi viongozi serikalini tumeuza eneo, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa," alisema Kiungani.
Hadi jana mchana vurugu zilikuwa zikiendelea na hakuna taarifa kamili ya hasara ambayo imepatikana. Mkuu wa wilaya hiyo alikuwa akiwaomba viongozi wa serikali ya kijiji cha Singisi kuwasihi wananchi kuacha vurugu hizo.
Je, una maoni yapi?

[ 1 Maoni ] ( 2 waliosoma mpaka sasa ) | makala hii na maoni
Tujielekeze Katika Kutambua na Kuthamini Jitihada za Kweli Badala ya Kurubuniwa na Kukumbatia Uongo
Monday, 8 June, 2009, 12:53
Wapo watu katika jamii yetu ambao huruka na mitazamo yao dhidi ya uongozi na serikali ni potofu, wanajitwisha sifa ya kuwa mabingwa wa kusambaza uongo katika nchi yetu. Wamekuwa wanaishutumu Serikali na vyombo vyake kuwa imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa Watanzania za kupambana na maovu dhuluma na rushwa, na kuegemeza shutuma hizo kwa kutumia neno linaloshabikiwa sana siku hizi, ufisadi. Huu si mtazamo sahihi kwa kuwa serikali ni yetu na hipo kwa niaba yetu na inayoyafanya ni kwa manufaaa kwa Watanzania wote, ni wajibu wa kila Mtanzania kwanza kutambua kwamba waliopewa dhamana ni wanaadam wanapaswa kutiwa moyo pale wanapofanya vizuri na wanapaswa kulaumiwa pale wanaposhindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo. Lakini lawama hizo lazima ziende sambamba na amoni, ushauri, na lugha ya kuhamasisha na kuwatia moyo ili kuzipa pengo la upungufu uliopo na hapohapo kuimarisha ari yao ya kufanya vizuri na zaidi.
Uongo huu unapoenezwa na watu wazima tena wenye akili timamu kwa sababu za maslahi yao ya kisiasa huku wananchi wa Tanzania wakishuhudia kazi kubwa inayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wetu Mhe, Jakaya Mrisho Kikwete. Hii ni aibu kubwa kwa kila Mtanzania na kwa Taifa letu pia.Watanzania tunapaswa tuelewe kwa pamoja kwamba tabia na mwenendo wa kujishutumu hata tunapofanya vizuri miongoni mwa Mataifa ya jirani zetu tukishindwa sisi kutambua ubora tunayoyafanya atudhoofishi serikali ya Rais Kikwete wala chama chake bali tunajenga hisia za kujidhoofisha na kamwe mwendelezo wa hisia na fikra hizo utarithiwa pia na vizazi vya Taifa letu na matokeo yake yanaweza kuwa mabaya zaidi kwa sababu kwanza yanapunguza ari, yanajenga na kuimarisha hisia za kutokujiamini na kutoamini wengine. Hali hiyo ndiyo inayoziathiri baadhi ya nchi za wenzetu ambazo ziliwahi kuwa imara na madhubuti lakini baada ya kuboromoka zimeshindwa kurudi kwenye hali yake kwa miaka lukuki.
Serikali ya Rais Kikwete ilikabiliwa na misukosuko mingi tokea kipindi inaingia madarakani kufuatia wimbi kubwa la uhalifu nchini lililohusisha wizi na uporaji wa fedha katika mabenki, mauaji ya wafanyabiashara wa madini yaliyoundiwa tume iliyozaa shauri dhidi ya aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai ambalo shauri hilo liko mahakamani hadi hii leo.
Serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Kikwete ilidhamilia kutekeleza kwa dhati nia yake ya kupambana na rushwa kwa kutumia uzoefu uliokwisha patikana katika awamu tatu zilizopita kwa ujasiri mkubwa na kwa misingi ya utawala wa sheria.
Imepigana na kupambana na rushwa ndogo na rushwa kubwa. Imechukua hatua kali na madhubuti kuhusu vitendo vya rushwa vilivyofanywa kwa nyakati tofauti kipindi kilichopita na sasa.
Dhamira thabiti ya Rais Kikwete kupambana na rushwa ilijionyesha dhahiri tokea mwanzo kabisa mwa uongozi wake. Katika hotuba yake ya kuzindua Bunge jipya Desemba 30, 2005, mjini Dodoma, siku tisa baada ya kuapishwa kuwa Rais, Mhe. Kikwete alisema:
“Tutaongeza kasi ya kupambana na rushwa kisayansi kwa kushambulia kiini chake, na kuziba mianya yake… Tutaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya rushwa hususan Taasisi ya Kuzuia Rushwa, Jeshi la Polisi na Mahakama…Ndugu zangu, naomba tuwe waadilifu. Tusilaumiane.”
Ni dhamira hiyo iliyowezesha Utawala wa Rais Kikwete kukabiliana na rushwa kubwa kubwa bila aibu, woga wala kusita. Katika kipindi kifupi tu cha miaka minne, Rais Kikwete amefanya maamuzi makubwa ya kukabiliana na rushwa kubwa kama ifuatavyo:
(a) Tokea mwishoni mwa mwaka jana, watu 21 wamefikishwa kortini wakikabiliwa na kesi kubwa 13 za Malipo ya Akaunti ya Nje (EPA - External Payment Accounts) katika Benki Kuu ya Tanzania. Kesi hizo zinaendelea mahakamani.
(b) Viongozi waandamizi watatu wa zamani wa Serikali, wakiwamo mawaziri wawili na Katibu Mkuu mmoja, wamefikishwa kortini wakikabiliwa na kesi ya kutumia vibaya madaraka yao na kuliingizia taifa hasara wakati wakiwa madarakani. Kesi yao inaendelea.
(c) Maofisa waandamizi wawili wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wako kortini wakikabiliwa na kesi ya kuliingizia taifa hasara kutokana na gharama za ujenzi wa minara pacha ya Benki hiyo.
(d) Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri kadhaa nchini ama wamefukuzwa kazi ama kufikishwa kortini wakishitakiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
(e) Taasisi mbalimbali zilizoko mstari wa mbele katika kupambana na rushwa zinaendelea kuchunguza kesi mbili zinazohusishwa na rushwa kubwa.
(f) Mikataba mbalimbali iliyofikiriwa kuwa chanzo mojawapo kikubwa cha rushwa kubwa imeanza kuchunguzwa na hatua zimeanza kuchukuliwa kuziba mianya ya rushwa katika mikataba hiyo.
Hata pale ambako hapakuwapo na ushahidi wowote wa dhahiri wa uvunjwaji wa sheria ama maadili, ama palihitajika Serikali ya Rais Kikwete kuthibitisha kuwa inajali utawala bora na uwajibikaji, imechukua hatua bila kusita.
Mfano mzuri ni uamuzi wa Rais Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri aliloliteua mwenyewe na kukubali kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa Februari, mwaka jana.
Hivyo, katika kipindi cha miaka mitatu na miezi mitano, Rais Kikwete ameonyesha na kuthibitisha uhodari wake wa kupambana na maovu hayo katika jamii bila woga na kwa uhodari mkubwa. Anatimiza kwa dhati ahadi yake ya kupambana na rushwa ya aina zote kubwa na ndogo na matumizi mabaya ya madaraka ya umma. Amekuwa kiongozo hodari na asiye tetereka katika maamuzi makubwa na ya msingi yanayohusu umma wa Watanzania, amethibitisha dhahiri na kwa vitendo kusimamia na kutekeleza ilani ya chama chake bila woga huku akitambua kwamba akiyafanya hayo anaungwa mkono na Wanachama wa chama chake waliomkabidhi bendera ya kuzinadi sera na ilani kwa Watanzania.
Jambo la msingi na muhimu kwa wananchi ni kuendelea kumuunga mkono Rais Kikwete katika mapambano hayo makubwa na makali dhidi ya rushwa. Mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa dhati wa wananchi kwa kuwa yeye ndiye jemedari na Watanzania wote tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya, ambayo ushindi ni lazima. Ni muhimu kusisitiza kuwa hii ni hatua ya awali tu mapambano bado yanaendelea kwa kasi ile ile.
“Lakini yote haya hayatapata mafanikio makubwa endapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo vyetu vilivyokabidhiwa jukumu hilo (kupambana na rushwa). Ushirikiano huo kutoka kwa wananchi ni wa lazima.”
Rais Kikwete na Serikali yake ya awamu ya nne wameonyesha na kuthibitisha kuwa walidhamilia kwa dhati kuwatumikia wananchi lakini kubwa zaidi ni ujasiri wa Rais wetu wa kuongoza mapambano hayo kama alivyokuwa akitoa ahadi wakati akiomba ridhaa ya Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi. Rais wetu amestahili pongezi za dhati tuendelee kumpa kila aina ya ushirikiano.
CCM inastahili pongezi kwa kutekeleza Ilani yake kwa umahiri na ustadi mkubwa, aidha inapaswa ijivunie kwa kutoa kiongozi bora, hodari na makini aliyeonyesha na kuthibitisha waziwazi kwa kila Mtanzania kuwa amejitoa kuwatumikia wananchi. Lazima Watanzania tutambue kwamba maslahi ya Taifa letu hayana mfano wake ushabiki wetu wa Kisiasa ulenge na kuimarisha Umoja wetu, Uzalendo wetu na Utaifa wetu. Sisi Watanzania heshima yetu ni umoja na umadhubuti wa Taifa letu hadhi na heshima yetu vitabaki kulindwa na kila Mtanzania kwa gharama yoyote. Nayasema haya bila woga, bila aibu nikitambua kwamba wajibu wa kulisemea Tanzania ni wa kila Mtanzania popote alipo.
Mwisho.
Mwamnyahenza Rajab
[ Weka Maoni ] | makala hii na maoni
CCM huree Busanda
Saturday, 30 May, 2009, 12:15
Na Gazeti la Uhuru
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemtangaza mgombea ubunge wa jimbo la Busanda kwa tiketi ya CCM, Lolesia Bukwimba, kuwa mshindi baada ya kuwabwaga wapinzani wake watatu.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Daniel Mollel, alisema Lolesia amepata kura 29,242 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, mgombea wa CHADEMA, Finias Magessa, aliyepata kura 22,799.
Wagombea wengine walioshiriki katika uchaguzi huo ni Beatrice Lubambe wa UDP aliyepata kura 271 na mgombea wa CUF, Oscar Ndalahwa aliyepata kura 977.
Mollel kwa mujibu wa kifungu cha 81 A cha sheria ya uchaguzi, alimtangaza Lolesia baada ya kuwabwaga wapinzani wake hao.
"Kutokana na ushindi huu, namtangaza Lolesia Bukwimba wa CCM kuwa mshindi halali wa uchaguzi mdogo jimbo la BusandaÉendapo kuna mgombea mwenye malalamiko atapewa fomu kama ilivyo kawaida ili aweze kukata rufani," alisema Mollel.
Akizingumza muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Lolesia alisema anawashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua na kuwaahidi kuwa atafanya kazi kwa bidii.
"Nimeupokea ushindi huu kwa furaha na ninawashukuru wananchi wa Busanda kwa kunichagua, nawaahidi nitawatumikia wote," alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Hasna Mwilima, alimpongeza Lolesia kwa kuchaguliwa, ambapo pia alimshauri kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi zao kama Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyotaka.
"Nampongeza sana Lolesia kwa kuchaguliwa, pia namkumbusha kuwatumikia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao kama Ilani ya CCM inavyoelekeza," alisema Hasna.
Wananchi wa jimbo hilo nao walisema wameupokea ushindi wa Lolesia na CCM kwa jumla kwa furaha, ambapo pia waliwataka wagombea walioshindwa kujipanga kwa uchaguzi ujao.
Mwananchi ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini, alisema ushindi huo unaashiria CCM inazidi kukubalika nchini.
Uchaguzi huo ulitokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge, Faustine Rwilomba, Februari mwaka huu, akiwa kwenye matibabu nchini India.
Katika kampeni za uchaguzi wa Busanda, kila chama kilitumia mbinu zake, ambapo CHADEMA waliamua kutumia helikopta kwa nia ya kuibuka na ushindi.
Mbali ya kutumia helikopta, CHADEMA iliwahi kufanya operesheni maarufu kwa jina la sangara na ambayo matokeo ya uchaguzi yanaonyesha haikuwa na matunda yoyote ya maana.
[ 2 Ongeza Maoni ] ( 4 waliosoma mpaka sasa ) | makala hii na maoni
Ikulu yawabana makatibu wakuu
Saturday, 30 May, 2009, 12:04
Na Mwananchi
BAADA ya kuwazuia wabunge kuwa wajumbe kwenye taasisi za kifedha, mianya ya ufisadi imezidi kubanwa baada ya Ikulu kuandaa waraka ambao utawaondoa makatibu wakuu wote katika nafasi za uenyekiti wa bodi za mashirika ya umma.
Katikati ya wiki, gavana wa Benki Kuu (BoT), alitoa maagizo kuwa taasisi za kifedha za umma hazitaruhusiwa kuwateua wabunge kuwa wajumbe wa bodi za taasisi hizo ili kuondoa mgongano wa kimaslahi.
Kwa mujibu wa duru za habari za kuaminika, agizo la Ikulu limetolewa na katibu mkuu kiongozi, Philemon Luhanjo. Habari hizo zinasema hatua hiyo imefikiwa ili kuondoa mgongano wa kimaslahi katika utumishi wa umma.
Kaimu msajili wa hazina, Geoffrey Msella alikiri jana kuwa alipata taarifa za waraka huo, lakini akasema hajapata barua rasmi kutoka kwa katibu mkuu kiongozi.
"Nafikiri, inawezekana amewaandikia kwanza makatibu wakuu wenyewe na baadaye anaweza kuleta kwetu, lakini hadi sasa (jana) sijapata taarifa rasmi," alisema Msella.
Alipoulizwa kuhusu waraka huo, Luhanjo alisema hakuwa katika nafasi nzuri kuzungumza. "Siwezi kuzungumza kwa sasa nipo kwenye mkutano," alisema Luhanjo kwa kifupi jana jioni.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe alikiri kupata taarifa hizo alipohojiwa na Mwananchi, lakini akasema si rasmi bali amesikia.
Kutolewa kwa waraka huo wa kudhibiti watendaji hao wakuu wa wizara ni moja ya hatua kubwa za serikali katika kuimarisha utawala bora na kuondoa mgongano wa kimaslahi.
Baadhi ya makatibu wakuu ambao ni wenyeviti wa bodi za mshirika ya umma hadi sasa, ni pamoja na Bliandina Nyoni wa Wizara ya Afya. Kwa sasa, Nyoni ni mwenyekiti wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF).
Mwingine ni Ramadhan Kijjah ambaye kwa sasa ni katibu mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi. Kijjah ni mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi wa Pesheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na Mfuko wa Jamii kwa Watumishi wa Serikali (PSPF).
Kwa mantiki hiyo, makatibu wakuu watabaki kuwa wajumbe wa bodi kutokana na mwingiliano wa shughuli za kiutendaji.
Una maoni yapi?
[ Weka Maoni ] | makala hii na maoni
Wabunge waondolewa ulaji
Saturday, 30 May, 2009, 11:47
Na Habari Leo
Wabunge wameanza kunyang’anywa sehemu ya ulaji kutokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa waraka unaowaelekeza wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye bodi za mashirika na taasisi za fedha kuondolewa mara moja. Hatua hiyo inatokana na ushauri uliotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kushauri wabunge wasiwe wajumbe wa mashirika yoyote ya umma, ili kuondoa mgongano wa maslahi. Kaimu Msajili wa Hazina, Godfrey Sella, alisema jana kuwa utekelezaji wa waraka huo wa BoT unaanza mara moja. Alisema kuna baadhi ya wabunge wenye maslahi katika taasisi za kifedha; hivyo si vizuri viongozi hao kuwa sehemu ya bodi za wakurugenzi.
Tayari BoT imetoa orodha ya wabunge wote ambao ni wajumbe kwenye taasisi za fedha na imepeleka waraka huo kwa Msajili wa Hazina ili aondoe majina ya wabunge hao kwenye bodi hizo. “Lengo hapa ni kutenganisha usimamizi na utekelezaji…tumepata waraka huo wa BoT na kinachofuata ni utekelezaji,” alisema Sella wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), aliyehoji sababu ya wabunge wapigwe marufuku kuwa wajumbe wa mashirika ya umma wakati kuna baadhi yao wana uwezo.
Mbunge huyo alisema kama kuna chama cha siasa kimeshinikiza suala hilo ni vyema kikapuuzwa; kwa kile alichodai kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki wabunge, kwani nao ni sehemu ya jamii. “Kuna wabunge wana uwezo mkubwa wa kuisaidia Serikali kupitia mashirika haya, iweje waondolewe kwenye nafasi zao za ujumbe wa bodi za mashirika ya umma?” alihoji mbunge huyo. Baada ya swali hilo, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto, alifafanua kuwa hakuna chama cha siasa ambacho kimekuwa kinashinikiza suala hilo; ila ni ushauri uliotolewa na ofisi ya CAG.
Ndipo Kaimu Msajili wa Hazina akafafanua, kwamba tayari hatua zimeanza kuchukuliwa na akaeleza kuwa zina nia nzuri ya kuwafanya wabunge wawe wasimamizi wazuri wa mashirika hayo. Wakati huo huo, Msajili huyo wa Hazina alikiri kuwa kampuni za Meremeta na Buhemba hazijawasilisha hesabu zozote katika ofisi yake kwa kile alichodai kuwa wizara ndiyo yenye jukumu la kuomba hesabu hizo. Alisema Meremeta ambayo iko chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, haina hesabu zozote lakini pia BoT ambayo inahusika na kampuni hiyo nayo haina hesabu zake.
“Hii inahesabika kama ni kitegauchumi cha serikali, lakini kwa mtazamo wangu, si shirika la kitega uchumi kwani hata CAG ameshindwa kuifanyia ukaguzi, kwa vile haina mali inayoonekana kwa macho,” alisema Sella. Kuhusu majukumu ya ofisi ya Msajili wa Hazina, Kaimu Msajili huyo alilalamika kuwa ofisi yake imejikuta wakati mwingine ikifanya kazi za ndani za mashirika ya umma kutokana na mfumo wa kiutendaji uliopo. Alisema kwa sasa wanajitahidi kuandaa waraka utakaosaidia kufanya mabadiliko ili ofisi ya Msajili wa Hazina ibaki kuwa msimamizi wa mashirika ya umma bila kuingilia utendaji wa mashirika hayo.
“Tunataka sisi tubaki kusimamia na kuona kama uamuzi unaofanywa na mashirika haya unazingatia maslahi ya taifa,” alisema. Hata hivyo alisema kwa sasa wizara nyingi ambazo zinatakiwa zipeleke mapendekezo ya wajumbe wa bodi wa mashirika mbalimbali kabla ya kutangazwa, hazifanyi hivyo. Alisema licha ya sheria kuzitaka kufanya hivyo kwa makusudi, mawaziri wanakaidi. “Ukihoji utaulizwa Msajili ni nani na ukisema ufuate sheria lazima utagongana na wakubwa zako, ndiyo maana tunaamua kukaa kimya.”
Je, Una maoni yapi?
[ 1 Maoni ] ( 4 waliosoma mpaka sasa ) | makala hii na maoni
Hisia za Uzanzibari, Utanganyika ndizo zitauzamisha Muungano
Thursday, 14 May, 2009, 16:24
Maoni ya Mhariri wa Nipashe
mekuwa kama ada, kila uchao kuna jambo jipya linajitokeza kama moja ya changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwelekeo wa siku za hivi karibuni unatoa picha kwamba Muungano wa nchi hizi mbili ni kama umejengwa juu ya urafiki wa kutokuaminiana.
Inawezekana uhuru wa kutoa maoni kwa njia za uwazi zaidi umetoa fursa kwa watu wengi zaidi kuzungumzia kasoro zilizoko katika Muungano wa huu, hali ambayo miaka kabla ya 90 haikuwako.
Tunaamini kwamba watu kuwa na uhuru wa kuzungumzia Muungano na changamoto zake ni njia moja sahihi ya kujenga; kwa maana kwamba kama udhaifu ukijulikana na kuzungumzwa basi watu watakuwa tayari kutatua hitilafu hizo. Wahenga walisema kujua tatizo ni nusu ya kupata utatuzi wake.
Pamoja na changamoto zote zinazoweza kutajwa kuwa ni kero hasa za Muungano, uamuzi wa hivi karibuni wa kuwataka Watanzania wenye asili ya Bara kulipa kodi ya ardhi ya Dola za Marekani 5,000 kwa mwaka sawa na raia wengine wa kigeni, hakika ni kielelezo kwamba wapo watu wanaochokonoa kadri wawezavyo ili kuudhoofisha Muungano!
Maamuzi haya yanadaiwa kuwa yanatokana na sheria ya ardhi ya mwaka 1992 ya Zanzibar ambayo inamtaja Mzanzibari pekee kuwa na haki ya kumiliki ardhi visiwani humo, wengine wote wanahesabika kama wageni, yaani hata Watanzania wanaotoka Bara wanatambuliwa kama wageni!
Kutokana na sheria hiyo, Watanzania kutoka Bara waliolowea na kujiendeleza Zanzibar kwa miaka, wakapata kipande cha ardhi na kuiendeleza sasa watalazimika kulipa kodi hiyo kwa mwaka kama walivyo wageni wengine wowote kutoka kona yoyote ya dunia hii.
Haya yakitokea Zanzibar, sheria za ardhi namba nne na tano za Tanzania za mwaka 1998, zinahalalisha kila Mtanzania kuwa na haki ya kumiliki ardhi. Mtanzania huyu aweza kuwa yule wa kuzaliwa au wa kuomba; wote wanaruhusiwa kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kigezo hiki kinawapa hata Wazanzibari haki ya kumiliki ardhi Bara.
Tunatambua kwamba wapo Wazanzibari wengi tu wajasiriamali waliobobea wamejiendeleza na sasa wanamiliki si tu ardhi, bali mali za uhakika zisizohamishika Tanzania Bara. Hawa wana haki kabisa mbele ya sheria kumiliki wanachomiliki na kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi, sisi tunawatia shime wawekeze zaidi na zaidi kwa ajili ya ustawi wa nchi yao.
Lakini wakati tukitambua sheria na hali halisi ya ardhi kwa pande zote za Muungano, yaani Zanzibar yenye ardhi finyu na Tanzania Bara yenye ardhi kubwa na fursa nyingi, tunapatwa na wasiwasi kwamba kwa nini katika kipindi hiki ambacho Muungano unapita katika kipindi cha majaribu makubwa, suala la kuwaweka kundi moja Watanzania wa Bara kundi moja na wageni linawekewa mkakati?
Tunashindwa kujua kama kweli msukumo pekee wa kuwaweka Watanganyika katika kundi la wageni visiwani Zanzibar ni matokeo ya mahitaji ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya visiwa hivyo, au ni njia nyingine ya mapambano kama nyingine nyingi ambazo zimeshuhudiwa katika siku za hivi za karibuni za Zanzibar kutaka kujionyesha kwamba ni taifa linalojitegemea?
Tunasema haya si kwa sababu tunaunga mkono mbinu zozote mbaya za kukandamiza haki za Wazanzibari, ila tunasukumwa na kitu kimoja; kwamba baada ya miaka 45 ya Muungano kila uchao tofauti zinatafutwa, kukuzwa na kupigiwa mbiu kana kwamba kufanya hivyo ndiyo njia ya kuujenga.
Tunapata hofu kwamba kama viongozi wetu wasipokaa kitako na kutafakari kwa mapana mambo yanayotengenezwa, kusukumwa na kupigiwa kampeni kuhusu udhaifu wa Muungano, kuna kila dalili kwamba huko tuendako mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Tunafikiri huu si wakati wa kuendelea kubaguana baina ya Wazanzibari na Watanganyika, pia si wakati wa kuhoji nani ananufaika zaidi na kwa nini, ila kwa upeo wetu tunaamini huu ni wakati wa kushikamana zaidi, kuvuta kwa pamoja zaidi na kurekebisha kasoro zilizopo hata kama ni za kisheria ili kujenga Muungano imara zaidi. Tujitahidi kutibu kuliko kuendelea kubomoa.
[ Weka Maoni ] | makala hii na maoni
Safari ni Ndefu: Baada ya Busanda ni Biharamulo!!!!
Thursday, 14 May, 2009, 10:21
Habari Leo (15.05.2009)
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mwingine mdogo katika Jimbo la Biharamulo Magharibi utakaofanyika Julai 5 mwaka huu. Uchaguzi huo ulitangazwa jana Dar es Salaam huku kampeni za vyama vya siasa zikiendelea wilayani Geita kwa ajili ya uchaguzi mwingine mdogo utakaofanyika mwezi huu jimboni Busanda.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu kwa waandishi wa habari, uteuzi wa wagombea utafanyika Juni 9 na kampeni zitaanzia Juni 10 hadi Julai 4 mwaka huu. Jimbo hilo lilikuwa wazi tangu Oktoba 12 mwaka juzi, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutengua matokeo ya uchaguzi na hivyo Mbunge aliyekuwapo kwa tikiti ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), Phares Kabuye kupoteza kiti chake.
Hata hivyo, Kabuye ambaye alifariki dunia mwezi uliopita, hakuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo alikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania. Wakati mchakato wa rufaa hiyo ulikuwa haujakamilika, Kabuye alikufa katika ajali ya basi mkoani Morogoro wakati akienda Dar es Salaam kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TLP.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema alisema chama chake kinajipanga kuhakikisha kinamweka mgombea makini atakayeendeleza historia ya kuongoza jimbo hilo.
Mrema aliviomba vyama vya upinzani kujenga umoja ili kukiwezesha chama chake kupata mwakilishi bungeni kwa kile alichoeleza kwamba TLP inafahamika na kukubalika kwa kiwango kikubwa jimboni humo. “TLP tulikuwa na katoto kamoja, kamekufa...tunaomba ushirikiano wa upinzani uanzie Biharamulo Magharibi kama hatua ya kumwenzi Kabuye,” alisema Mrema.
Je, Una maoni yapi?
[ Weka Maoni ] | makala hii na maoni
Mambo ya Busanda
Thursday, 14 May, 2009, 10:12
Mwananchi 14.05.2009
Kampeni za uchaguzi wa ubunge Busanda zinazidi kuwa moto baada ya mkutano wa chama cha UDP kumalizika kwa watu kutawanyika huku wakimzomea Mwenyekiti wa chama hicho, John Momose Cheyo wakati akimtambulisha mgombea wao Beatrice Lubambe.
Mkutano huo ambao umefanyika katika eneo la Katoro jana ulimalizika kwa watu waliokuwa wamejaa wakimsilikiliza kusambaa huku wakipiga mayowe kumzomea alipoanza kumtambulisha mgombea wa chama chake.
Huo ni mkutano wa kwanza wa chama hicho tangu kuanza kwa kampeni hizo Aprili 29, mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa UDP hawakuzindua kampeni zao rasmi kwa sababu ya kukabiliwa na ukata wa fedha.
Mkutano huo ambao ulianza na watu wachache, lakini baadaye waliongezeka kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele na kusikiliza kwa makini.
Hata hivyo mambo yaliharibika baada ya Cheyo kuanza kumwaga sera zake akisema wakimchagua mgombea wa UDP atateuliwa na kuwa mbunge ambapo atasimamia maendeleo ya eneo hilo pamoja na kuhakikisha kuwa bei ya pamba inapanda hadi kuwa Sh1,000 kwa kilo moja tofauti na bei ya sasa ya Sh 400.
“Nimezungumza kwa saa nzima mnanisikiliza sijatukana mtu, lakini wanasiasa wengine wanatukana hovyo hapa jukwaani, jambo hili haliwezi kufanya tulinde amani na uhuru wa kisiasa uliopo,” alieleza Cheyo.
Wakati huo wananchi walikuwa wametulia na kumsikiliza kwa makini, lakini alipomsimamisha mgombea wake walishika mikono kichwani na kumzomea kwa kupiga mayowe ya “uuwiiii”, huku wakitawanyika.
Kutokana na hatua hiyo Cheyo na mgombea wake walilazimika kuufunga mkutano wao na kuondoka haraka wakihofia kutokea vurugu.
[ 1 Maoni ] ( 7 waliosoma mpaka sasa ) | makala hii na maoni
SMZ yazidi kuubomoa Muungano yataka bara walipe kodi ya ardhi
Sunday, 10 May, 2009, 10:41
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza mkakati mpya wa kuwataka wawekezaji na watu wenye asili ya Tanzania Bara kusajiliwa na kuanza kulipa kodi ya ardhi ya dola za Marekani 5000 (Sh6.5 milioni), kila mwaka kwa kila hekta moja ya ardhi.
Hata hivyo, SMZ ilisema mwekezaji mwenye asili ya Zanzibar atapaswa kulipa dola 500 (Sh650,000).
Mpango huo umetangazwa jana na Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mohammed Hashim Ismail kufuatia bodi hiyo kupewa uwakala wa kusimamia na kukusanya kodi ya ardhi.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Zanzibar ya mwaka 1992, Mzanzibari tu ndiye mwenye haki ya kumiliki ardhi, lakini wageni wote wanapaswa kukodishwa wakiwemo watu wenye asili ya Tanzania Bara.
“Hatua hii itatuwezesha pia kuwafahamu wamiliki wote wakubwa na wadogo wadogo wa vipande vyote vya ardhi hapa Zanzibar pamoja na wale ambao wanatajwa kuhodhi maeneo kinyume na utaratibu,” alisema kamishna huyo.
Alisema hatua hiyo itawasaidia kuwatambua wasiokuwa Wazanzibari na kuishauri serikali kuchukua hatua zinazofaa.
Kamishna huyo alisema viwango vya malipo vitapitiwa upya ili viende na wakati na kuishauri serikali juu ya hatua sinazostahili kuchukuliwa.
Alisema ardhi ni suala muhimu katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi wa Zanzibar, ndio maana serikali imeamua kuhakiki upya viwanja vya makazi kupitia mradi wa SMOLE.
Kamishna huyo alisema kupitia mradi huo taarifa zote zitaingizwa katika mfumo wa kompyuta ili kuweza kuwatambua watu wote waliokodishwa ardhi.
Hashim Ismail alisema kwamba bodi ya mapato imeanza kujitayarisha kwa ajili kukusanya fedha hizo pamoja na kuwatambua waliopewa ardhi kinyume cha sheria.
Hata hivyo zoezi hilo linatarajiwa kuibua mjadala mkubwa kutokana na ukweli kwamba, inachochea ubaguzi kati ya Watanzania Bara na Wazanzibari hivyo kuendelea kuudhoofisha muungano.
[ Weka Maoni ] | makala hii na maoni
Mbele
